Wananchi wakiwa katika foleni wakisubiri kununua mafuta katika moja ya vituo vinavyouza nishati hiyo jijini Dar es Salaam.(Picha na Evance Ng'ingo).
NAIBU Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto, amewataka wafanyabiashara wa mafuta wawauzie wananchi mafuta, na wasipofanya hivyo hadi saa 12 jioni leo wanyang’anywe leseni, na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) likavifungue vituo hivyo ili mafuta yapatikane.
Zitto amelieleza Bunge kuwa, ni lazima ionekane kuna Serikali, kuna dola na sheria zinatekelezwa.
Zitto ametoa msimamo huo leo wakati akichangia mjadala wa dharura kuhusu hali mbaya ya upatikanaji wa mafuta nchini iliyosababishwa na mgomo wa wafanyabiashara wa mafuta uliodumu kwa takribani wiki moja sasa.
Zitto amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inapaswa kuwaagiza wafanyabishara wa mafuta kwamba leo lazima wawauzie wananchi mafuta.
“Ewura iwaode (iwaagize) wafanyabiashara wa mafuta… hatuwezi kukubali… leo mafuta yatoke” amesema Zitto na kubainisha kwamba, uamuzi huo unaweza kusababisha shida kwa wananchi lakini wamezizoea.
“Ni lazima ionekane kuna Serikali, ni lazima ionekane kuna dola, ni lazima kuwepo usimamizi wa vyombo vya Serikali” amesema na kuwaponda wafanyabiashara wa mafuta kwamba, wakati Serikali ilipopandisha bei ya mafuta ya taa, hawakuhoji, kesho yake nao wakapandisha, lakini sasa bei imeshushwa wanagoma.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), amesema, wafanyabiashara wa mafuta wanaonesha ubabe na jeuri ya fedha hivyo Serikali ichukue hatua kwa kuwa ina wajibu wa kuwalinda raia wake.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika amesema, Serikali ina asilimia 50 ya hisa katika Shirika la BP, lakini nao wamegoma kuwauzia wananchi mafuta, Serikali ipo wapi?
Mnyika amesema, Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuchukua hatua kumaliza tatizo la lafuta, na ana ushahidi kwamba, baadhi ya maofisa wa Serikali wanahusika katika suala hilo kwa kuwa wamehongwa.
Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela, amesema, wafanyabiashara wa mafuta wasidhani kwamba wapo juu ya sheria na wanapaswa kuiheshimu Serikali.
Mbunge huyo amesema, Ewura na Serikali wanapaswa kuonesha meno, na ameunga mkono kauli ya Zitto kwamba, ikifika saa 12 jioni leo, wananchi wawe wanauziwa mafuta kama kawaida.
Kwa mujibu wa Malecela, hana uhakika kama ni kweli wafanyabiashara wa mafuta wanapata hasara, na wanapaswa kutambua kuwa unapofanya biashara lazima uchukue ‘risk’.
Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF), ameunga mkono kauli ya Zitto kwamba, wafanyabiashara wakiendelea kugoma kuuza mafuta, JWTZ iingilie kati, na amesema, kuna taarifa kwamba viongozi wa Serikali wanafanya biashara ya mafuta, hivyo tatizo la sasa liwe fundisho kwa Serikali.
Mnyaa amesema, si busara kwa Serikali kujitoa katika kufanya biashara zote, na amesema, Bunge limeshindwa kuisimamia Serikali, kwa kuwa, hadi sasa hakuna kamati ya kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Bunge.
Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama, amesema, Serikali isipochukua hatua kumaliza tatizo la mafuta, haitaheshimiwa.
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeshangaa kwa nini Serikali haijasema chochote kuhusu tatizo hilo na imemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atoe tamko kuhusu hali mbaya ya upatikanaji wa nishati hiyo.
Hali ya upatikanaji wa mafuta nchini ni mbaya, na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, January Makamba, katika baadhi ya maeneo lita moja inauzwa Sh. 3,000/-, 4,000/- na 5,000/-.
Makamba amesema, lengo la Serikali kushusha bei ya mafuta ilikuwa ni kushusha gharama za maisha lakini hali imekuwa tofauti kwa sababu kuna udhaifu katika usimamizi wa sheria. Mbunge huyo amesema, bei ya mafuta lazima ishuke kati ya leo hadi kesho asubuhi.
Amesema, Serikali inapaswa kuonesha kuwa ipo na ina uwezo wa kusimamia sheria, na kwamba, Serikali inapaswa kutoa tamko kwa kuwa mafuta ni muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi. “PM(Waziri Mkuu) sema kitu” amesema Makamba.
“Nataka Serikali ijaribu kuonesha kuwa ipo… tunaposema nchi itasimama ni kweli itasimama ” amesema Makamba na kuhoji kwamba, tangu mwaka 2,000 Serikali imekuwa ikipanga bei za mafuta, kwa nini limekuwa tatizo sasa?
Kwa mujibu wa Makamba, tatizo la mafuta halijapewa uzito unaostahili, na kwamba limeshughulikiwa tofauti na matarajio ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
0 Comments