Mkakati huo wa kumshambulia Zombe umeanza rasmi jana ambapo Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, John Mwambigija, aliwasomea mamia ya wananchi wa kata ya Ruanda jijini Mbeya walioshiriki mkutano wa hadhara wa chama hicho, hotuba ya kambi ya upinzani ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Akisoma hotuba hiyo kwa wananchi ambayo alidai imeletwa mkoani Mbeya ikitokea Dodoma, alisema Zombe hana sababu za kuanza kumshambulia Mbunge wa Arusha, Lema kuhusu yeye (Zombe) kushutumiwa kuhusika na mauaji ya wafanyabiashara wa Morogoro.
Mwambigija alisema Zombe anapaswa kutambua kuwa Lema alisoma hotuba hiyo siyo kwamba yalikuwa ni mawazo yake binafsi bali yalikuwa ni ya kambi ya upinzani ambapo yeye (Lema) aliiwasilisha kwa sababu ni Waziri kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alidai yeye (Mwambigija) alishaishi Dar es Salaam na kwamba alimfahamu Zombe jinsi alivyokuwa na mtandao wa majambazi na kwamba kwa kuwa Zombe alikuwa mfanyakazi wa Jeshi la Polisi na alifahamu kuwa Godbless Lema alikuwa katika mtandao wa wezi wa magari je alichukua hatua gani.
Alisema Chadema inamheshimu sana na Watanzania wapenda amani wanampenda Mbunge wa Arusha, Lema na ndiyo maana alichaguliwa kwa kura nyingi na kushika nafasi ya pili kitaifa nyuma ya mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliyeshika nafasi ya kwanza.
Mwambigija ambaye wakati akihutubia wananchi wa kata ya Ruanda huku akisoma nakala ya hotuba ya bajeti ya Kambi ya Upinzani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya mwaka 2011/2012, alisema katika mikutano yao yote watakayokuwa wakiifanya katika mkoa wa Mbeya watahakikisha wanamwelezea Zombe kuwafahamisha Watanzania jinsi anavyodaiwa kushiriki katika mauaji ya wafanyabiashara wa Morogoro hata kama ameshinda kesi.
Mapema Julai 31, mwaka huu Mkuu wa Upelelezi wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam, Zombe ameibuka tena na kutoa kauli kwa kudai kuwa siku Chadema kikiingia madarakani yeye atajinyonga na kumshutumu Mbunge wa Arusha, Lema kwamba alikuwa kwenye mtandao wa wizi wa magari.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments