KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen ametangaza kikosi cha wachezaji 20 kwa ajili ya mechi ya kirafiki wiki ijayo, huku kipa mahiri nchini Juma Kaseja akiachwa. Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, Stars itacheza ugenini Agosti 10 mwaka huu tarehe ambayo inatambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (Fifa). Akizungumza jijini Dar es Salaam, Poulsen aliwataja wachezaji hao kuwa ni makipa, Shabani Dihile (JKT Ruvu) na Shabani Kado (Yanga).

Mabeki ni nahodha Shadrack Nsajigwa (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Amir Maftah (Simba), Chacha Marwa (Yanga) na Juma Nyoso (Simba).
Viungo ni Shaaban Nditi (Mtibwa Sugar), Juma Seif ‘Kijiko’ (Yanga), Jabir Aziz (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Soud Mohamed (Toto Africans) na Godfrey Taita (Yanga). Washambuliaji ni Salum Machaku (Simba), Julius Mrope (Yanga), Mrisho Ngassa (Azam), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), John Bocco (Azam) na Thomas Ulimwengu (U23). Kaseja pia aliachwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza na Jamhuri ya Afrika ya Kati Juni mwaka huu na Stars kufungwa mabao 2-1.


Mchezaji Mohammed Banka ambaye alikuwepo kikosi kilichocheza na Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Bangui, pia ameachwa katika kikosi cha jana.


Kuhusiana na mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’, Poulsen alimtaka mchezaji huyo kuwa na nidhamu ili aweze kuitwa Taifa Stars siku zijazo.


Poulsen alisema licha ya mchezaji huyo kuwa na uwezo wa kucheza soka anatakiwa kutambua nidhamu ndio itakayomuwezesha kufika mbali na kuwa mchezaji bora zaidi.


Alisema kwa sasa hawezi kumuita mchezaji huyo kwa kuwa anaonekana ana tatizo la nidhamu lakini aliahidi kumwita katika mechi zijazo iwapo akionesha nidhamu.


Poulsen pia alimtaka mchezaji Thomas Ulimwengu kutafuta timu ya kuchezea ili pia kuweza kupata nafasi ya kuchezea timu ya taifa kwa mechi zajazo.


Pia aliwataka wachezaji waliotajwa katika kikosi hicho kufika leo mazoezini Uwanja wa Karume kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo, ambayo hata hivyo bado haijajulikana watacheza na timu gani.


Poulsen pia amesema hakuwaita kwenye kikosi chake wachezaji wanaocheza soka nje ya Tanzania kwa sababu ni mechi ya kirafiki na kuwa atawaita siku zijazo.


“Timu itaingia kambini kesho (leo) jijini Dar es Salaam na itaanza mazoezi siku hiyo hiyo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.


“Msafara wa timu hiyo wa jumla ya watu 30 utaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano,” alisema Wambura.