MBUNGE wa Konde, Khamis Said Haji amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki itavunjikia Zanzibar ikiwa Wakenya hawataacha mara moja kununua kwa magendo karafuu itokayo Zanzibar.

Amesema pamoja na hilo, Wakenya pia wamekuwa hawawathamini Watanzania wanaotoka
visiwani humo hasa wafanyabiashara na maagizo ya Balozi Mdogo wa Tanzania, Mombasa, hawayajali.

Hayo yalisemwa juzi bungeni na Haji wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya mwaka 2011/2012 iliyowasilishwa bungeni na Waziri mwenye dhamana, Samuel Sitta. 

“Wanapokea karafuu za magendo kutoka Zanzibar bila kujali, wananunua na kuziandika kuwa zinatoka kwao, sisi tukinunua kwa magendo meno ya tembo kutoka kwao, watabaki na tembo hao, naomba serikali iingilie kati,” alisema Haji.

Aliongeza, “Karafuu pekee inatoka Zanzibar, lakini kimataifa ipo inayoonekana inatoka Mombasa, Kenya, wataacha lini kutufanyia hivi?

“Mbona sisi tunawaheshimu lakini wao hawatuheshimu? Waje wanunue kwa utaratibu uliopo kupitia shirika la ZSTC na si vinginevyo, Wabunge wote wa Zanzibar tunaumia na hili, serikali msikae kimya.”