Bendera ya Visiwa vya Sao Tome

Wapiga kura nchini Sao tome na Principe wamemchagua kiongozi wa wakati wa uhuru wa Taifa dogo la Afrika Magharibi kuwa Rais.
Manuel Pinto da Costa, mchumi wa ‘Ki-Marxist’ aliongoza visiwa hivyo viwili kwa miaka 15 ya mwanzo baada ya uhuru kutoka kwa utawala wa mkoloni wa Kireno mwaka 1975.
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1991, Rais amegawana madaraka na Waziri Mkuu.

Kisiwani Sao Tome.

Bw Pinto da Costa, mwenye umri wa miaka 75, alipata ushindi mwembamba dhidi ya mgombea kutoka chama cha Waziri wake mkuu katika duru ya pili ya uchaguzi siku ya Jumapili.
Evaristo Carvalho, ambaye ni spika wa bunge alipata asilimia 47 ya kura.
Eduardo Lobao, mwandishi wa shirika la Habari la Ureno Lusa, amekieleza kipindi cha BBC cha Network Africa kuwa wakazi wengi wa visiwa hivyo wapatao 165,000 ni vijana na hawana kumbukumbu za enzi za utawala wa chama kimoja wa Bw da Costa.

Lakini wanatarajia Rais Mteule kuweka shinikizo kadhaa kwa serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Patrice Trovoada – kutatua baadhi ya matatizo ya nchi, anasema.
Kampeni za Bw Pinto da Costa zililenga katika utengamano wa kisiasa na aliahidi kupambana na ufisadi ulioasambaa.
Visiwa vya Sao Tome na Principe,vilivyokuwa mwanzoni wazalishaji wa kwanza kwa kakao vina utajiri wa mafuta na uzalishaji wa kibiashara utaanza miaka michache ijayo.
Hata hivyo umezuka mjadala juu ya namna gani matumizi yake yatafanyika na kusababisha hali tete ya kisiasa.