Bei za hisa duniani zimeshuka kwa kiasi kikubwa huku kukiwa na hofu kuhusu mwelekeo wa uchumi duniani.
Mjini New York, bei ya hisa za Dow Jones zilianguka kwa pointi mia tano kiasi kikubwa zaidi kushuhudiwa kwa karibu miaka mitatu.
Kushuka kwa bei ya hisa kumesababishwa na mgogoro wa madeni ya mataifa wanachama wa bara Ulaya huku ikiofiwa kuwa huenda Italy na Uhispania zitakabiliwa na matatizo hayo.
Pia kuna hofu kwamba huenda Marekani ikakumbwa na mdororo mwingine wa kiuchumi.
Mwandishi wa BBC mjini New York anasema kengele ya kuashiria kufungwa kwa soko la hisa mjini New York liliwapa afueni wafanyibiashara ambao siku nzima walishuhudia mauzo yakishuka kwa kasi mno.
Ikiwa chini ya miaka mitatu tangu msukosuko wa kiuchumi duniani kushuhudiwa sasa wasiwasi umezuka kuwa hali hiyo huenda inarejea.
Matukio haya bila shaka sio zawadi nzuri kwa Rais wa Marekani Barack Obama ambaye leo anasheherekea miaka 50 tangu azaliwe, na hasaa wakati uchaguzi unanukia.
Wawekezaji nchini Marekani na kote duniani wamekuwa wakiuza hisa zao na badala yake kubana pesa zao au kununua hati za dhamana za serikali ya Marekani.
Hofu kuhusu kasi ya kuimarika kwa uchumi wa marekani na pia kujikokota kwa uchumi wa nchi zingine za magharibi pia ni baadhi ya sababu za kuporomoka kwa bei za hisa.
Wadadisi wanasema kuwa hali hii huenda ikawa mbaya zaidi wakati serikali ya Marekani itakapotangaza takwimu zinazoonyesha viwango vya ukosefu wa ajira nchini humo. Dalili zinaonyesha kuwa takwimu hizo sio za kufurahisha.
0 Comments