MCHEZO wa kirafiki kati ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya Sudan umefutwa.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura amesema kuwa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA) kimefuta mechi hiyo iliyokuwa ifanyike kesho jijini Khartoum, Sudan.
“Uamuzi huo umetokana na wakala wa mechi hiyo Hadi Sharkawy kushindwa kupata kwa wakati tiketi ya kuisafirisha Taifa Stars kwenda Khartoum.

“Pia kutokana na mechi hiyo kufutwa, kambi ya Stars iliyokuwa hapa Dar es Salaam nayo imevunjwa leo,” alisema Wambura.

Mechi ya Stars na timu ya Taifa ya Sudan ‘Nile Crododile’ ilianza kuingia kwikwi mwishoni mwa wiki, baada ya TFF na Yanga kuanza kugombea wachezaji, ambapo TFF ilikuwa ikisisitiza wachezaji wa Yanga walioitwa Stars waripoti, huku Yanga ikiamua kuondoka nao.



Hatua ya mwisho timu hizo zilikubaliana Yanga itangulie na wachezaji hao na jana wangejiunga na Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Sudan, lakini Stars juzi ilikwama kuondoka, jana pia haikusafiri ikaeleza ingesafiri leo ambayo pia imeota mbawa.

Wachezaji hao wa Stars waliotangulia na Yanga ni Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub, Chacha Marwa, Juma Seif na Godfrey Taita.

Julius Mrope yeye aliachwa katika kikosi cha Yanga kilichoondoka juzi, hivyo alibaki kambini Stars.

Wakati huohuo, Yanga imeanza vibaya ziara yake nchini Sudan baada ya kufungwa mabao 3-1 na wenyeji wao El Hillal.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Luis Sendeu bao la Yanga lilifungwa na Hamis Kiiza na kuwa leo Yanga itacheza na El Merreikh mchezo mwingine wa kirafiki.

Katika hatua nyingine Wambura alisema kuwa, kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji kilichofanyika mwishoni mwa wiki ilizungumzia suala la mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ kutoitikia mwito wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen kucheza mechi kati ya U23 na Shelisheli zilizofanyika Arusha na imeamua kuliacha suala hilo kwa kocha kwa vile kuna maagizo ametoa kwa mchezaji huyo.

“Poulsen amemtaka Boban binafsi kwenda kumueleza sababu ya kutoitikia mwito wake wa kucheza mechi dhidi ya Shelisheli kabla hajafanya uamuzi mwingine kuhusu mchezaji huyo,” alisema Wambura.