Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumisi wa Umma), Hawa Ghasia.
Kambi ya Upinzani Bungeni imesisitiza kuwa serikali ina uwezo wa kuwalipa wafanyakazi wa umma kima cha chini Sh. 315,000 kama ina dhamira ya dhati ya kuwajali wafanyakazi.
Msemaji Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Regia Mtema, aliyasema hayo wakati akisoma hotuba ya kambi hiyo kuhusiana na makadirio ya bajeti ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka 2011/12.
Alisema Kambi hiyo iliitaka serikali ipandishe kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma hadi kufikia Sh. 315,000, ili kuwawezesha wafanyakazi kumudu gharama za msingi za maisha.
“Cha kusikitisha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, pamoja na mambo mengine, alisema kuwa baada ya kukokotoa Bajeti Mbadala ya Upinzani, alibaini kuwa Wafanyakazi wote wa umma wakilipwa kima cha chini cha Sh. 315,000, serikali italazimika kutumia jumla ya Sh. trilioni 7,9 kwa mishahara tu na kwa hiyo itakuwa imebakiwa na fedha kidogo ambazo hazitatosha kununulia madawa, na kugharamia huduma nyingine muhimu kwa wananchi zinazotolewa na serikali,” alisema na kuongeza:
“Ukweli ni kuwa kauli hii ya Mhe Waziri wa Utumishi haikuwa na dhamira njema ya kuwasaidia Wafanyakazi waliopendekeza ongezeko hilo la mshahara.”
Alisema wakati akihutubia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam mwezi Aprili mwaka 2010, Rais Jakaya Kikwete, katika maelezo yake alisema wafanyakazi wote wa sekta ya umma wanakadiriwa kuwa 350,000.
Alisema hata wakisema kuwa ndani ya mwaka mmoja uliopita idadi ya wafanyakazi wa sekta ya umma imeongezeka hadi kufikia wafanyakazi 400,000, bado kima cha chini cha Sh.315,000 kikilipwa, Serikali haiwezi kutumia jumla ya Sh. trilioni 7.9 kama alivyodai Waziri wa Nchi, ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumisi wa Umma), Hawa Ghasia.
Alisema Serikali ikilipa kima cha chini cha sh 315,000 kwa wafanyakazi 400,000, bila kuzingatia asilimia 15% ya makato ya akiba (kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii – PPF, PSPF, LAPF na NSSF) na asilimia 3% ya makato Bima ya Afya (NHIF), itatumia jumla ya Sh. trilioni 1.512 tu kwa ajili ya mishahara na sio shilingi trilioni 7.9 alizodai waziri.
Alisema hata kama kima hicho cha Sh. 315,000 kitalipwa kwa wafanyakazi 400,000 pamoja na kujumuisha asilimia 15% ya makato ya akiba (kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii – PPF, PSPF, LAPF na NSSF) na asilimia 3% ya makato Bima ya Afya (NHIF), kwa pamoja (na gharama za huduma nyingine – OC), bado gharama nzima ya kulipia mshahara huo, haiwezi kuzidi shilingi trilioni mbili .
Alisema gharama hizo ni kwa mujibu wa hesabu zilizopigwa na wataalamu wazalendo wa Vyuo vikuu vya ndani na kuthibitishwa na Kambi rasmi ya Upinzani.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments