|
Bi,Rebecca Barila akiingia Mahakamani. |
Miongoni mwa habari zinazotawala magazeti ya Uingereza ni habari ya mwanasayansi maarufu katika utafiti wa maambukizi ya HIV Ukimwi kumgeuza mtumwa mwanamke raia wa Tanzania kwa kumfanyisha kazi kwa miezi sita bila ya kumlipa chochote huku akimtesa.
Rebecca Balira, mwenye umri wa miaka 47 ambaye pia ni mwanasayansi katika mojawapo ya taasisi zinazoongoza duniani kwa tafiti za HIV jijini London, Uingereza, amepandishwa kizimbani akituhumiwa kumgeuza mtumwa msichana wa kitanzania Methodia Mathias mwenye umri wa miaka 21.Rebecca alimchukua Methodia toka Tanzania kama mfanyakazi wa ndani akimwahidi mshahara wa paundi 96 sawa na Tsh. Laki mbili na nusu kwa mwezi.
(Mshahara wa chini ambao angeweza kumlipa ni angalau Tsh. Milioni 1 na laki 6).Pamoja na ahadi za mshahara huo kiduchu kwa maisha ya gharama ya jiji la London, Methodia hakulipwa chochote kwa miezi sita aliyokuwa akifanya kazi za ndani kwa bi Rebecca akifanya usafi wa nyumba, akipika na kufua pamoja na kuwalea watoto watatu wa bi Rebecca.
Mbali ya yote Methodia aliambulia mateso huku akinyang'anywa pasipoti yake ili asikimbie pamoja na kukatazwa asipige simu nyumbani Tanzania au kuwasiliana na mtu yoyote yule hapa Uingereza au huko Tanzania.
Kali ya yote ni kwamba Methodia alilazimishwa kulala kitanda kimoja na mtoto wa kiume wa bi Rebecca mwenye umri wa miaka 12. Baadhi ya shuruba alizopata ilikuwa ni kila siku za jumapili wakati walipokuwa wakienda kanisani ambapo Rebecca na watoto wake walipanda basi huku Methodia akitakiwa atembee kwa miguu hadi kanisani.
Maelezo haya yalitajwa mahakamani kama vielelezo vya bi Rebecca kumgeuza mtumwa msichana wa Kitanzania aliyemtoa Tanzania na kumfanyisha kazi bila malipo kwa miezi sita.
Kesi hii ilifika mahakamani baada ya Methodia kufanikiwa kumuelezea mwanamke aliyejuana naye hapa Uingereza kuhusiana na mateso aliyokuwa akipata akipigwa makofi na mateso pamoja na sidiria yake kukatwa vipande vipande kwa mkasi na bosi wake huyo siku alipokasirika.
Mwanamke huyo ndiye aliyewapa taarifa polisi ambao waliamua kuichunguza kesi hiyo na hatimaye kumfikisha kizimbani bi Rebecca.
Mahakama iliambiwa kuwa Rebecca ambaye kwa miaka 15 amekuwa akifanya kazi kwenye taassisi ya London School of Hygiene and Tropical Medicine, ndiye aliyeandaa viza ya Methodia pamoja na kumlipia tiketi ya ndege toka Tanzania.
Methodia aliwasili Uingereza mwezi februari mwaka jana na kuishi na Rebecca pamoja na watoto wake watatu kwenye nyumba ya vyumba viwili jijini London ambapo Rebecca alikuwa akilala chumba kimoja na watoto hao akilala kitanda kimoja na mtoto wa kiume.
"Unapofikiria Utumwa unaweza kufikiria watumwa wa kuchuma pamba kule Georgia, Marekani au biashara ya utumwa barani Afrika, hapa tunamzungumzia bi Rebecca Balira ambaye alimchukua Methodia kuishi kwenye himaya yake huku akimnyima huru wa kutembea na uhuru wa kufanya kile akipendacho", alisema mwendesha mashtaka wa kesi hiyo bi Caroline Haughey.
"Tunachoweza kusema hapa ni kwamba Rebecca Balira alimweka Methodia Mathias,msichana wa Kitanzania mwenye umri wa miaka 21 kwenye mazingira ambayo hayana tofauti na utumwa", aliendelea kusema bi Haughey.
"Alilazimishwa kufanya kazi kwa masaa mengi kwa siku na hakulipwa hata senti moja, alinyang'anywa pasipoti yake na aliwekwa kwenye mazingira ambayo hayakubaliki kwa wakati huo au sasa", aliendelea kusema mwendesha mashtaka huyo.
"Alilazimishwa kuamka saa 11 alfajiri kuandaa kifungua kinywa na chakula cha mchana kwaajili ya bi Rebecca atakapokuwa kazini, na bi Rebecca alipoondoka kwenda kazini alitakiwa kuwaamsha na kuwahudumia watoto na kuwapeleka shule watoto wawili wa mwanzo na kisha kubaki nyumbani akimtunza mtoto wa mwisho wa Rebecca huku akifanya usafi wa nyumba, akifua nguo kwa mkono, mchana alimpeleka mtoto huyo shule ya chekechea na kisha alienda kuwachukua toka shule watoto wa Rebecca na kurudi nyumbani ambapo aliandaa chakula cha jioni kwaajili ya watoto hao na kisha kuandaa chakula kingine cha jioni kwaajili ya Rebecca. Kwa kawaida alimaliza kazi za ndani saa tano usiku au saa sita na ndipo alipoenda kulala akisubiri kuamshwa tena saa 11 alfajiri", mahakama ya Southwark Crown Court iliambiwa na mwendesha mashtaka huyo.
Kwa upande wake Rebecca alijitetea akisema kuwa Methodia ni binamu yake na amekuwa akimhudumia vizuri tofauti na mashtaka aliyofunguliwa mahakamani.
Alikanusha mashtaka ya kumtesa kwa kumshambulia na kumgeuza mtumwa Methodia.
Kesi hii iliahirishwa hadi siku zijazo na itaendelea kusikilizwa tena mahakamani hapo.
Source- NIFAHAMISHE. |
|
|
0 Comments