Maelfu ya raia India wamejitokeza mitaani kumunga mkono mwanaharakati wa kupinga ufisadi Anna Hazare.
Awali wafuasi wa Bw Hazare walikusanyika nje ya jela mmoja mjini Delhi ambako amekuwa akizuiliwa tangu jumanne.Bw Hazare amegoma kuondoka katika jela hilo hadi serikali ya India itakapo mruhusu kutekeleza mpango wake kususia kula chakula hadharani.
Mwanaharakati huyo anahurumiwa na wengi nchini India na tayari maandamano ya kumuunga mkono yanazidi kuvutia idadi kubwa ya watu kote nchini humo.
Bw Hazare anashinikiza kufanyika kwa mageuzi katika sheria za kupambana na rushwa na alikuwa amepanga kuanza kukesha bila chakula ili kushinikiza hilo lifanyike.
Watu wengi wanaomuunga mkono wamejitokeza na mabango huku wakikemea serikali wakitaka aachiwe huru.
Raia hao wa India wanasema lazima serikali ichukue hatua za kukabili ufisadi uliokithiri nchini humo.
Hata hivyo waziri mkuu wa India Manmohan Singh amemkosoa mwanaharakati huyo akisema, ingawa nia yake ni nzuri anatumia dhana potufu kulazimisha bunge lifuate matakwa yake.
Mshirika wa karibu wa Bw Hazare amesema kuwa sasa amekubali kuondoka jela baada ya polisi kuridhia kuwa anaweza kufanya mgomo huo wa kususia chakula kwa siku kumi na tano kwenye bustani mmoja mjini Delhi.
Bw Hazare na wafuasi wake 1,200 walitiwa nguvuni na polisi wakiwa kwenye bustani ya JP park saa chache kabla waanza kusisia chakula.
Mwezi April, Bw Hazare alivunja mgomo wake wa kususia chakula baada ya siku nne pale serikali ilikubali kuwa anaweza kuhusika kuandaa mswada wa kupambana na ufisadi nchini humo ambapo kutakuwa ofisi maalum ya kuchunguza wanasiasa na watumishi wa serikali wanashukiwa kuhusika na ufisadi.
Mwanaharakati huyo mwenye miaka 74, hata hivyo anapinga mswada uliowasilishwa bungeni kwa kuwa waziri mkuu na majaji hawata chunguzwa.
0 Comments