Ben akiwa na jezi ya Bafanabafana.

Mshambuliaji kutoka Afrika Kusini Benni McCarthy ameingia mkataba wa kuichezea klabu ya Orlando Pirates, hali inayokamilisha miaka 14 ya kuishi na kucheza soka Ulaya.
Ben hapo alipokuwa Blackburn Rovers.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusinic - Bafana Bafana ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 33, siku ya Jumanne amejiunga na klabu hiyo ya Johannesburg kwa mkataba wa miaka miwili.

"Benni ni mchezaji aliyepata mafanikio makubwa na ni mwana kandanda anayetambuliwa nchini Afrika Kusini kwa miaka mingi," Mwenyekiti wa Pirates Irvin Khoza alieleza kupitia mtandao wa klabu hiyo.

"Tumefurahi sana ameamua kujiunga nasi."


McCarthy amekuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na klabu ya West Ham kutenguliwa kutokana na makubaliano ya pande mbili mwezi wa Aprili.

Tangu alipoondoka klabu ya Cape Town Spurs mwaka 1997, McCarthy alichezea vilabu kadha vya Ulaya akianzia na Ajax Amsterdam nchini Uholanzi.

Baada ya kuichezea klabu ya Celta Vigo ya Hispania, alikwenda Ureno ambako alichezea timu ya Porto, ambapo akiwa na klabu hiyo waliweza kunyakua ubingwa wa Ligi ya Uefa mwaka 2004, kabla hajaelekea England.

Alichezea Blackburn Rovers kabla ya kujiunga na West Ham, ambapo huko alimalizia soka yake kutokana na kuongezeka uzito.

Uwezo wake wa kusakata soka uliposhuka na pia matatizo ya uzito yalimsababishia McCarthy kutochaguliwa katika kikosi cha Bafana Bafana kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, zilizofanyika kwao nchini Afrika Kusini.