Rais Jakaya Kikwete amewataka wakuu wa wilaya nchini zinazoonyesha dalili za uhaba wa chakula watoe habari haraka ili ziweze kupatiwa chakula kwa sababu taifa linalo chakula cha kutosha.
Aidha, Rais Kikwete amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna Mtanzania yeyote ambaye atapoteza maisha kwa njaa kwa sababu tu ya kuwepo kwa dalili ya njaa ama ukosefu wa chakula katika eneo lolote la Tanzania kwa sababu taifa lina chakula cha kutosha kabisa.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo kwa wakuu wa wilaya, na ahadi hiyo kwa wananchi, wakati alipozungumza juzi, wakati anafuturisha viongozi na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwenye Ikulu Ndogo ya mjini Shinyanga.

Aliwasili mkoani hapa jana kwa ziara ya siku mbili mkoani humo na miongoni mwa mambo mengine ameshiriki katika mazishi ya Luteni Jenerali (mst) Silas Peter Mayunga kwenye Makaburi ya Wasabato ya Unyanyembe mjini Maswa.
Akijibu shukurani za Sheikh Mkuu wa Mkoa, Sheikh Ismail, Rais Kikwete amesema kuwa amepata habari na kujionea mwenyewe wakati anasafiri kwa gari kwenda Maswa kumzika Jenerali Mayunga kuwa zipo dalili za waziwazi za ukame ambao unaambatana na ukosefu wa chakula.
“Nimejionea mwenyewe hali ya ukame wakati wa safari yangu kwenda Maswa. Sikuona dalili yoyote ya vifurushi vya akiba ya chakula ambayo kwa kawaida ni dalili ya akiba ya chakula cha kutosha katika mkoa huu. Leo sikuona.”
“ Lakini napenda kuhakikishieni ndugu zangu kuwa tunacho chakula cha kutosha kabisa kuhudumia kila eneo lenye uhaba wa chakula nchini. Hakuna Mtanzania ambaye atakufa kwa njaa kwa sababu chakula kiko cha kutosha kabisa,” alisema.
Hata hivyo, Rais alisema kuwa ili Serikali iweze kujua haraka mahitaji halisi ya maeneo yenye dalili za uhaba wa chakula ama tayari upo uhaba, ni lazima wakuu wa wilaya watoe taarifa haraka kwa mamlaka husika ili wananchi waweze kupelekewa chakula mara moja.
“Nataka kuwaambieni wakuu wa wilaya kuwa hakuna aibu yoyote kwa nyie kusema kuwa maeneo yenu yana tatizo la njaa. Aibu itakuwa mkuu wa wilaya akikaa kimya kiasi cha wananchi katika eneo lake kuanza kupoteza maisha kwa sababu ya uhaba wa chakula. Hili hatutalivumilia. Mkuu yoyote ambaye ataona aibu kusema eneo lake lina njaa na watu wetu wakapoteza maisha, huyu tutamshughulikia,” alisema.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI