MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Mussa Aboud Jumbe amesema Serikali haitowavumilia watu wanaoendesha uvuvi haramu ambao ni tishio kwa matumbawe na mazalio ya samaki.

Jumbe alisema hayo jana alipokutana na kamati za uvuvi za Huba ya Minai na kusema mswada mpya wa uvuvi unatoa adhabu kali kwa wavuvi watakaoendesha uvuvi haramu katika maeneo ya hifadhi.

“Jamani mimi nawakumbusha tu wavuvi wa mwambao wa pwani kwamba ni marufuku kuvua samaki kwa kutumia mitego ambayo haikubaliki...uvuvi haramu haukubaliki katika maeneo ya hifadhi,” alisema Jumbe. 

Alisema baadhi ya maeneo ya hifadhi yamekumbwa na tatizo la ukosefu wa samaki. Baada ya kuwepo kwa vitendo vya uvuvi haramu ambavyo vimeharibu matumbawe pamoja na mazalia ya samaki.

Uvuvi haramu wa kutumia baruti pamoja na nyavu zenye macho madogo kwa kiasi kikubwa umeleta athari kubwa ikiwemo upungufu wa samaki, ambao umevikumba visiwa vya Unguja na Pemba katika siku za hivi karibuni.