Maige alisema Serikali pia imeimarisha kikosi dhidi ya ujangili katika Kanda ya Kaskazini, Arusha kwa kuwaongezea wafanyakazi vitendea kazi, na kufanya mabadiliko kwa baadhi yao.
“Baada ya tukio hilo, tumekamata watuhumiwa sita na kuwafungulia mashitaka ya uvunjaji wa sheria ya wanyamapori,” Maige alisema.
Alisema pamoja na upelelezi wa Polisi juu ya kesi hiyo, vyombo vya Ulinzi na Usalama vinafanya uchunguzi ndani na nje ya nchi.
Vyombo vya nje ya nchi vilivyohusishwa ni pamoja na Shirika la Kimataifa la Kulinda Wanyamapori na Viumbehai Vilivyo Hatarini Kutoweka (CITES).
“Uchunguzi huo pia unakusudia kujiridhisha kama kuna ushiriki wa watumishi wa Wizara. Wizara yangu imeunda kikosikazi cha kukagua mazizi ya wanyamapori na ndege wanaosubiri kusafirishwa yanayomilikiwa na wafanyabiashara 180 wenye leseni,” alisema.
Wakati huo huo, Serikali imesema itakamilisha mchakato wa ugawaji vitalu vya uwindaji wa kitalii mwezi ujao, tayari kuvigawa kwa watakaokuwa na vigezo vya kuviendesha.
Waziri Maige alisema hayo wakati akiwasilisha Makadirio ya Matumizi kwa mwaka 2011/12 ya jumla ya Sh bilioni 57.8.
Kwa mujibu wa Maige, ugawaji huo ni kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2018 utakaohusisha vitalu 159 vilivyotangazwa katika awamu mbili tofauti.
Alisema tayari wizara imeteua Kamati ya Ushauri kwa ajili ya kugawa vitalu hivyo.
Katika hatua nyingine, Maige alisema ujenzi wa makumbusho ya muda katika eneo la Laetoli kwenye Hifadhi ya Ngorongoro umekamilika na taarifa za utafiti zilizofanyika zimehifadhiwa.
|
0 Comments