Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar vimekamata shehena ya meno ya Tembo iliyokuwa imefichwa kwenye makontena mawili yaliyokuwa na dagaa katika Bandari ya Zanzibar.
Mkuu wa Bandari ya Malindi, Martin Lissu, alisema makontena hayo yalikamatwa jana mchana na kuongeza kuwa yalitokea Tanzania Bara yakidaiwa yalikuwa njiani kuelekea Malyasia.
Lisu alisema ndani ya makontena hayo kulikuwa na magunia ya dagaa ambapo kila gunia lilikuwa na vipande kati ya 8-10.
Alisema shehena hiyo iliwasili mjini Zanzibar wiki mbili zilizopita kwa Meli ya MV Break iliyotokea Tanzania Bara.
Taarifa kutoka Bandari ya Zanzibar zilisema watu wawili wanashikiliwa pamoja na wakala aliyepokea mzigo huo kutoka Bara.
Alisema baada ya kuwasili visiwani humo mzigo huo ulihifadhiwa eneo la Mwanakwelekwe ambapo kila moja lilikuwa na urefu wa mita 20.
Makontena hayo yalikuwa na magunia 135 ya dagaa ambayo inadaiwa yalitokea jijini Mwanza, lakini kabla hayajaondoka visiwani humo yalidakwa na vikosi vya usalama.
Taarifa zinasema mzigo huo ulikuwa unasafirishwa na raia wa China na kwamba watu waliokuwa wakisafirisha walikuwa wanatumiwa.