Chama cha Democratic na wapinzani wake Republicans wameridhiana

Bunge la Congress nchini Marekani limepitisha mswada ambao utadhibiti deni la nchi hiyo na kuepusha hatari ya serikali kukosa pesa.
Mswada huo sasa utawasilishwa mbele ya baraza la senate.
Baada ya wanasiasa wa marekani kutofautiana kuhusu kuongeza kiwango cha kukopa cha serikali, bunge la Congress hatimaye limepiga kura kuunga mkono mswada utakaowezesha serikali ya nchi hiyo kuongeza kiwango cha madeni yake.
Kufuatia kupitishwa kwa mswada huo, marekani haina wasi wasi tena kuwa itashindwa kufadhili shughuli zake kuanzia hii leo, kama ilivyokuwa imetangazwa na wizara ya fedha.

Mswada huo umepata kuungwa mkono na wajumbe wengi katika baraza la wawakilishi wakati ulipowasilihsiwa kupigiwa kura.
Kwa hivyo sasa umevuka kikwazo chake cha kwanza. Hata hivyo matokeo hayo hayakuwa suala ambalo lilishangaza.
Jambo ambalo lililokuwa geni ni kuwasili bungeni kwa mbunge wa congress Bi Gabrielle Giffords kwa mara yake ya kwanza tangu apigwe risasi kichwani mwezi January.
Wajumbe wa baraza la congress ambao wamekuwa wakivutana kwenye mijadala mikali walisimama kwa pamoja na kumshangilia alipowasili kupigia kura mswada huo.
Mswada huo ambao pamoja na kuongeza kiwango cha serikali kukopa fedha za kuendesha shughuli zake pia umependekeza hatua za kupunguza matumizi ya serikali.
Kuna kila uwezekano kuwa Rais Barack Obama atakuwa anatia saini kuudhinisha saa chache tuu kabla ya pesa zilizoko kwenye mfuko wa serikali kumalizika kulingana na ushauri wa wizara ya fedha.
Hapo jana Rais Barack Obama alitangaza kuwa chini ya makubaliano kati ya chama chake na kile cha Republicans serikali itapunguza matumizi yake kwa dollar trilioni moja katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Kwa wiki kadhaa, viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakivutana kuhusu njia bora ya kufuata kukabili madeni ya marekani.
Hali ambayo ilitishia kukwamihsa shughuli za serikali.
Rais Obama amesema kuwa mpango ulioafikiwa sio ule aliotarajia lakini amelazimika kuukubali ilikuwezesha huduma za serikali kuendelea na madeni yake yalipwe.
Utawala wa Rais Obama ulikuwa unakabiliwa na shinikizo kali kutoka kwa wapinzani kutoka chama cha Republican ambao walikuwa wanapinga pendekezo lake la kuwepo na mpango ambao utasitiri hali hadi mwisho wa mwaka ujao.
Chama cha Republicans kilitaka mpango huo uwepo hadi katikati ya mwaka ujao. Lakini sasa vyama hivyo vimekubaliana kuunda kamati maalum itakayotoa mapendekezo mapya mwezi Novemba.