Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal(Pichani juu), amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kutumia taasisi za fedha za ndani kwa ajili ya kuinua uchumi wao badala ya kungoja ruzuku kutoka nje.
Dk. Bilal ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi, baada ya kukagua shamba la zabibu lililoko katika kijiji cha Chinanganali II, Kata ya Bwigiri katika Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Alisema wananchi wanapaswa kujenga imani kuwa taasisi za fedha nchini zina uwezo mkubwa wa kusaidia wananchi kuondokana na umaskini kutokana na mikopo inayotolewa na taasisi hizo.
“Tutumie taasisi zetu za ndani kuinua uchumi, sio kuwa tegemezi kuongoja ruzuku kutoka nje. Dodoma tuna mifano mingi, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimejengwa kwa taasisi za ndani kwa asilimia 100,” alisema Dk. Bilal.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Lephy Gembe, alimweleza Makamu wa Rais kuwa Benki ya CRDB imetoa mkopo wa Sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kugharamia shamba hilo la zabibu la ekari 300.
Alisema mradi huo wa kilimo cha zabibu utawanufaisha wanachama wapatao 300 kutoka vijiji vya Buigiri, Chamwino, Manchali, Makoja, Mlebe na Chanangali II ambao kwa kutumia umwagiliaji wa matone watavuna wastani wa tani 10-15 kwa ekari kwa mwaka na kuweza kujipatia Sh. milioni 10 -15 kwa mwaka kwa bei ya sasa ya Sh. 1,000 kwa kilo ya zabibu.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments