Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange "Kaburu" (kushoto) na Mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga (kulia) wakiwa wameshika mikataba mipya baada ya kusaini pamoja na Mkurugenzi wa Masoko wa TBL,David Minja (wa pili kushoto) jijini Dar es Salaam. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah. (Picha na Yusuf Badi).

WADHAMINI wa klabu za Simba na Yanga Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro imetangaza mkataba mpya wa udhamini wa miaka mitano kwa klabu hizo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni tano.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo baina ya TBL na klabu hizo, Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, David Minja alisema kampuni hiyo imeamua kuingia mkataba mpya na klabu hizo baada ya mkataba wa awali wa miaka mitatu ulioonesha mafanikio kumalizika mwishoni mwa mwezi uliopita na hivyo wametoa mkataba mpya ambao umeboreshwa zaidi kimaslahi.


Kwa mujibu wa Minja katika mkataba huo mpya klabu hizo mbili zitapatiwa basi jipya kila moja lenye uwezo wa kuchukua abiria 54 , na pia gharama ya udhamini huo kwa kila timu ambao ulikuwa ni Sh milioni 16 kwa kila mwezi sasa umeongezeka na kuwa Sh milioni 25.



Aidha Minja alisema katika mkataba huo TBL itagharamia mikutano ya mwaka ya klabu hizo mbili zenye wapenzi wengi hapa nchini na pia klabu hizo zitapatiwa kila moja Sh milioni 20 kwa ajili ya shughuli ya kuandaa matamasha ya klabu hizo, ambapo Simba wataandaa tamasha linalojulikana kama ‘Simba Day’ ambalo litafanyika Agosti 8 jijini Arusha.


Mbali na hayo klabu hizo pia zitapatiwa vifaa vya michezo vyenye thamani kati ya Sh milioni 30 na 35 ambavyo vitatolewa mara mbili kwa mwaka kwa ajili ya kutumiwa na timu hizo kwenye michuano ya ligi na ile ya kimataifa.


Wakizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Lloyod Nchunga na Makamu wa Mwenyekiti wa klabu ya Simba Godfrey Nyange ‘Kaburu’ waliishukuru TBL kwa udhamini huo na kuahidi kutekeleza mkataba huo ili kujenga imani zaidi kwa mdhamini wao.


Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah mbali ya kuishukuru TBL kwa udhamini huo kwa klabu za Simba na Yanga amesema udhamini huo utazisaidia klabu hizo kufikiria zaidi masuala ya kiwanjani na kuongeza viwango vya timu zao kuliko kuangalia zaidi masuala ya gharama za uendeshaji wa klabu hizo.