Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, ameshuhudia maajabu wilayani hapa baada ya kukuta wanafunzi zaidi 380 wa Shule ya Sekondari Kate iliyopo wilayani hapa wanalazimika kulala madarasani kwa kutandika magodoro chini ya sakafu kutokana na shule hiyo kutokuwa na mabweni na vitanda.
Mulugo ambaye yupo katika ziara ya siku tano katika wilaya za Mkoa wa Rukwa, ameshuhudia maajabu hayo jana baada ya kuitembelea shule hiyo kuikagua kuangalia mazingira ya wanafunzi wanaposomea.
Mulugo baada ya kuwasili shule hapo alitaharuki baada ya kusomewa taarifa na Mkuu wa Shule hiyo, Amianie Manga, kwamba shule inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo wanafunzi kulala madarasani kwa kutandika magodoro sakafuni kutokana na shule kukosa bweni.
Manga alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002 yenye mchanganyiko wa wavulama na wasichana, wanafunzi walianza kulala madarasani kuanzia mwaka 2005 baada ya uongozi wa shule na kijiji kuamua kuibadili kutoka shule ya kutwa na kuwa ya bweni.

Manga alimweleza Mulugo kuwa, alipohamishiwa katika shule hiyo alikuta wanafunzi wanaendelea kulala chini madarasani na kwamba kwa kuwa suala hilo liliamuliwa na waliomtangulia kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za vijiji vya kata za Sintali na Kate ameshindwa kubadilisha utaratibu huo.
Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Joyce Mgana, alisema kilichosababisha hali hiyo ni kuigeuza shule hiyo kuwa ya bweni bila kuwa na matayarisho ya kujenga mabweni.
Mulugo baada ya kupata maelezo hayo, alipiga marufuku kuanzia jana wanafunzi wasilale madarasani hadi hapo utaratibu wa kujenga mabweni na kutengeneza vitanda utakapofanyika.
Aliwaagiza viongozi wa ngazi ya wilaya na kata kuitisha mkutano na wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ili kupanga mikakati ya kujenga mabweni.
“Napiga marufuku kuanzia leo (jana) wanafunzi wasilale tena madrasani, hili siyo ombi ni amri,haiwezekani wanafunzi wawe wanalala katika mazingira kama haya machafu, magorodo yamejaa vumbi,milango na madirisha mabovu,” alisema Mulugo.
Aidha, Mulugo aliamua kuendesha harambe ndogo ambapo zilipatikana Sh. 5,870,000 ambazo zitaanza kutumika kuyakarabati madarasa waliyoyatumia kulala wanafunzi wa shule hiyo.
Kwa upande wa wanafunzi Filbert Mwanaloya, Secilia Mwanandenje na Godluck Herman walisema wanapata taabu sana kulala madarasani sakafuni na kwamba mara kwa mara wamekuwa wakiugua vifua.
CHANZO: NIPASHE