JESHI la Polisi nchini limeanza kumtafuta nahodha wa meli ya mv Spice Islander iliyozama baharini katika eneo la Nungwi, Kaskazini Unguja usiku wa kuamkia Jumamosi.
Taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa jana na Mkuu wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, ilimtaja nahodha huyo kwa jina la Said Kinyanyite, ambaye ni mkazi wa Nzasa Mbagala, Charambe, Temeke, Dar es Salaam.
Mussa alisema nahodha huyo, ambaye hakuonekana baada ya ajali hiyo ni mzaliwa wa kijiji cha Mbwemkuru, Pande, Kilwa mkoani Lindi.
Kamishna Mussa aliwaomba wananchi kupitia mpango wa Polisi Shirikishi Jamii, kutoa taarifa kituo chochote cha Polisi endapo watapata taarifa za alikojificha, ili akamatwe na kutoa maelezo ya jinsi ajali hiyo ilivyotokea.
Taarifa hiyo ilisema tangu kuzama kwa mv Spice Islander, hajapatikana hali ambayo imewalazimu polisi kutafuta picha yake kwa lengo la kurahisisha utambuzi kwa watu wasiomfahamu wamwonapo.
Katika hatua nyingine, kazi ya kuopoa miili ya walionasa kwenye mabaki ya meli hiyo iliyokuwa ikifanywa kwa ushirikiano wa wapiga mbizi wa Afrika Kusini na majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, imeshindikana.
Ofisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, alisema kushindikana huko kumesababishwa na hali mbaya ya bahari na kina iliko meli hiyo tofauti na uwezo wa wazamiaji hao.
Inspekta Mhina alisema uamuzi wa kusitisha kazi hiyo ulitangazwa na Kamanda wa Operesheni hiyo wa Afrika Kusini, Wayne Combrink, aliyesema, wazamiaji wake na wa nchini, wameshindwa kuifikia meli hiyo baada ya kubaini kuwa iko kina cha zaidi ya meta 300. Uwezo wa wazamiaji hao ni kina kisichozidi meta 54.
Kwa hali hiyo, Kamanda alisema wameagiza nyambizi kutoka Afrika Kusini ili kuja kukamilisha kazi hiyo ambayo alisema isingewezekana kwa wazamiaji wenye zana za kawaida bila chombo hicho.
Wazamiaji hao waliwasili nchini Septemba 13 katika kundi la watu 16 wakiwamo madaktari wanne na vifaa vya kisasa wakidhani kina iliko meli hiyo kingekuwa chini ya meta 54.
Wakati huo huo, Nafisa Madai wa Idara ya Habari, Maelezo, Zanzibar, anaripoti kwamba jahazi lijulikanayo kwa jina la Asaa Robo lenye namba 328 likitoka Tanga kwenda Wete, Pemba lilizama jana asubuhi nje kidogo ya bandari ya Tanga.
Wafanyakazi tisa na nahodha waliokolewa na boti ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutoka Tanzania Bara lililokuwa likifanya doria ya kawaida.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo baada ya kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Rashid Bugi, Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu, alisema jahazi hilo lilibeba mizigo ya vyakula na magodoro mali ya Mkubwa Omari Saleh.
Alisema kuzama kwa jahazi hilo kulitokana na kugonga mwamba na kutoboka na kujaa maji.
Aidha, alivitaka vyombo vya baharini kuwa makini katika kupakia mizigo na kuhakikisha kuwa mizigo wanayochukua inalingana na uwezo wa vyombo.
Naibu Waziri alisema ni vyema vyombo hivyo vikazingatia sheria na kanuni ili kuepusha ajali za mara kwa mara, ambazo zinaweza kuepukika, ikiwa sheria zitafuatwa.
Gavu alitaja walionusurika katika ajali hiyo kuwa ni nahodha, Issa Sharifu Issa, mabaharia Hussein Saleh Omar, Ali Rashidi Ali, Ahmed Bakari Saleh, Ali Bakari Saleh, Hamad Rashid Ali na Abrahmani Bakari Othman.
Wengine ni Khamis Hamad Seif na Ali Sharif Ali ambao wote hivi sasa wamehifadhiwa katika gati kongwe ya kiwanda cha mbolea Tanga na hali zao zinaendelea vizuri.
Kutokana na ajali hiyo Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano imelazimika kuitisha kikao kati yao na wamiliki wa majahazi Jumatatu, kwa lengo la kuweka mikakati na kudhibiti hali kama hiyo isitokee.
Juzi, boti ya Sea Bus I ikitoka Pemba kuja Unguja ilishindwa kuendelea na safari, kutokana na hitilafu ya mitambo na kulazimika kurejea bandari ya Mkoani.
Nayo boti ya Sea Star iliyokuwa ikitoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam ililazimika kukatisha safari yake, mara tu baada ya kufika katika kisiwa kidogo cha Chumbe na kurejea bandarini Malindi, Zanzibar, kutokana na hitilafu ya mashine kuzima kutokana na mafuta kuingia maji.
0 Comments