Kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza kashfa ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti ya wizara hiyo tayari ilianz kazi jana.
Agosti, 26 mwaka huu, Spika wa Bunge, Anna Makinda, aliunda kamati hiyo yenye wajumbe watano itakayofanya kazi ya kuchunguza sakata nzima la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Kamati hiyo ilikutana jana asubuhi katika Ofisi ndogo za Bunge jijini chini ya Mwenyekiti wake, Ramo Makani, mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM). Wengeni ni Goesbert Blandes (Karagwe CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa
(Gando-CUF) na Martha Jachi Umbulla (Viti Maalum- CCM).
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, kamati hiyo ilikataa kuzungumza na waandishi wa habari.
Hata hivyo, kamati hiyo inafanya kazi kwa kuongozwa hadidu za rejea tano ikiwemo kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni na
kwamba, hadidu hiyo ya kwanza itakuwa na vipengele vitatu.
Vipengele hivyo ni kuchunguza uhalali wa utaratibu huo kisheria na kwa mujibu wa kanuni, iwapo fedha hizo huwa zinakasimiwa katika bajeti husika pamoja na matumizi halisi ya fedha zilizokusanywa.
Hadidu rejea ya pili ni kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uchunguzi alioufanya kuhusiana na agizo la Jairo kuchangisha fedha taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa Bajeti ya Wizara hiyo bungeni.
Vilevile, kuchunguza mfumo wa Serikali kujibu hoja zinazotolewa bungeni na taratibu za kualiarifu Bunge matokeo ya utekelezaji wa hoja hizo.
Ya nne ni kuchunguzwa kwa usahihi wa utaratibu uliotumiwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa suala la Jairo na kubaini iwapo utaratibu huo umeathiri dhana ya haki na madaraka ya Bunge.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments