Mechi hiyo itaanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hizo zote, Stars na Algeria iliyotua nchini juzi usiku, zina pointi nne na ili kufufua matumaini ya kushiriki AFCON 2012 zitakazoandaliwa kwa pamoja na nchi za Equatorial Guinea na Gabon, ni lazima zisake ushindi wa namna yoyote ile.
Akizungumza na gazeti hili jana, nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, alisema kuwa wamejiandaa vyema na wanachoomba ni dua za Watanzania kukamilisha malengo yao ya kuibuka na ushindi wa nyumbani.
Nsajigwa alisema kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao wamejipanga kupigana kufa na kupona na hiyo inatokana na kuimarisha kikosi chao pamoja na benchi la ufundi ikiwemo kuajiri kocha mpya Vahid Halilhodzic baada ya kumtimua wa awali, Rabah Saadane.
"Tunafahamu kwamba kesho (leo) tunakabiliwa na mtihani, tunaomba Mungu ili tushinde na kurejesha matumaini ya kufuzu fainali za Afrika," alisema nahodha huyo.
Alisema kwamba kila mchezaji amejipanga kucheza kwa juhudi na kwa kutumia faida ya uwanja wa nyumbani wanawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuwahamasisha zaidi.
Katika kudhihirisha kwamba mechi hiyo ni ngumu kwa pande zote mbili, jana mchana makocha, Jan Poulsen wa Stars na Halilhozic wa Algeria walishindwa kutokea katika mkutano wa waandishi wa habari kama ilivyopangwa awali na kila mmoja kueleza kwamba amebanwa na programu za kiufundi na kwamba watakuwa tayari kuzungumza baada ya kumalizika kwa mechi yao ya leo.
"Makocha wamesema kwamba wamebanwa na programu zao na hii inaonyesha ni jinsi gani mechi ya kesho (leo) ni muhimu, wamesema watakuwa tayari kuzungumza baada ya mechi hapo kesho (leo)," alisema Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mkutano huo kati ya makocha na wanahabari ulipangwa kufanyika saa 6:00 mchana lakini utakangazwa kuahirishwa hadi saa 8:00 mchana, na muda mfupi baadaye, Wambura akaeleza kwamba makocha hao hawataweza tena kuzungumza na vyombo vya habari.
Ili kuhakikisha ushindi unapatikana Poulsen amewaita nyota wote saba wanaocheza nje ya nchi ambao ni Athumani Machuppa, Mbwana Samatta, Nizar Khalfan, Henry Joseph, Danny Mrwanda, Abdi Kassim 'Babi' na Idrissa Rajab wakati Halilhodic amewaita wachezaji wa nje 20 na wa ndani wanne.
Mechi nyingine za Kundi D zinazotarajiwa kuchezwa leo ni Jamhuri ya Afrika ya Kati dhidi ya Morocco. Katika mechi nyingine za awali za kuwania kufuzu AFCON 2012, majirani Rwanda watawakaribisha Ivory Coast, Kenya watawavaa Guinea Bissau jijini Nairobi, Burundi watacheza nyumbani jijini Bujumbura dhidi ya Benin huku Uganda inayohitaji sare ili kufuzu watacheza ugenini dhidi ya Angola.
0 Comments