Ramadhan Semtawa
BAADA ya bei ya petroli kushuka kwa wiki nne mfululizo, leo bei ya bidhaa zinazotokana na nishati hiyo zitapanda na kudumu kwa wiki mbili zijazo.Safari hii petroli katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh 2,102 kwa lita moja ikilinganishwa na Sh 2,031 kwa bei, iliyoishia jana.

Kupanda na kushuka kwa bei ya nishati hiyo ya mafuta kwa lita, ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni ya ukokotoaji inayotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).




Wiki mbili zilizopita, Ewura ilitoa bei elekezi ambazo petroli ilishuka kwa Sh38.03 sawa na asilimia 1.84, dizeli Sh 45.15 sawa na asilimia 2.26 na mafuta ya taa bei ilishuka kwa Sh46.15 sawa na asilimia 2.33.

Hata hivyo, jana Ewura katika bei hizo mpya inayoanza kutumika leo imetangaza kupanda kwa bei ya rejareja ya petroli kwa Sh 70.12 sawa na asilimia 3.57 wakati dizeli imepanda kwa Sh 44.88 sawa na asilimia 2.38 na mafuta ya taa kwa Sh 33.02 sawa na asilimia 1.77.