Mamlaka ya vyombo vya baharini imesitisha safari zote za bahari kwa meli tano kutokana na meli hizo kukosa viwango vya kusafirishia abiria na mizigo.
Meli ambazo zimekatishwa safari ni MV Serengeti, Nura, Buraq One, Buraq Two na Mubarak. Meli hizo zilisajiliwa kwa ajili ya kusaidia kuvuta meli baharini na siyo kubeba abiria.
Mkurugenzi wa Mamlaka wa Vyombo vya Bahari Zanzibar, Haji Vuai Ussi, alisema katika taarifa yake kuwa kukatishwa kwa safari kwa vyombo hivyo kumetokana na vyombo hivyo kukosa usalama wa uhakika kwa abiria wake.
Aidha, amesema ingawa meli hizo zilianza kazi za kusafirisha abiria kwa muda mrefu, lakini zilishindwa kujisajili kwa kazi hiyo, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za vyombo vya baharini. 
Ussi alisema meli hizo pia zilikuwa zikihudumiwa na wafanyakazi wasiokuwa na sifa wala taaluma ya ubaharia pamoja na kushindwa kutoa taarifa za usalama kwa wasafiri wakati wanapokuwa safarini.
Ameongeza kuwa Mamlaka imebaini tatizo kubwa katika meli hizo mara baada ya kufanya ukaguzi na kugundua kuwa meli hizo zimekosa mfumo mzuri wa maasiliano pale ambapo linatokea tatizo la kiufundi.
Alisema mamlaka imegundua pia matatizo lukuki kwa manahodha wa meli hizo kwa kuondoa meli bila kujua taarifa za usalama wa abiria wao. (chanzo cha habari ni gazeti la nipashe na picha hazihusiani na habri.)