HATIMAYE aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (63), ametoka jela katika gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani.
Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika toka ndani ya familia yake jana, Liyumba alitoka gerezani hapo saa 3:30 asubuhi bila ya kuwepo kwa vikwazo vyovyote.
Vyanzo hivyo ambavyo havikutaka kutaja majina yao gazetini kwa madai kuwa wao si wasemaji wa familia ya Liyumba, vilisema kuwa ndugu zake wachache walifika saa mbili asubuhi katika gereza la Ukonga kwa ajili ya kumchukua ndugu yao.
Ilipofika saa 3:30 asubuhi, uongozi wa gereza hilo ulimruhusu Liyumba kutoka gerezani hapo baada ya kukamilisha taratibu zote za kumuachilia huru kisha wakafanikiwa kuondoka naye.
“Tunamshukuru Mungu ndugu yetu leo katoka gerezani baada ya kumaliza kifungo cha miaka miwili jela na hivi tuna furaha kwani amerudi uraiani na yote yaliyompata tunamwachia Mungu,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo juhudi za gazeti hili za kumpata Liyumba ili azungumzie kumalizika kwa adhabu yake, zilishindikana kufuatia ndugu zake wa karibu kueleza kuwa hivi sasa hayuko tayari kuzungumza na vyombo vya habari kwani anahitaji kupumzika pamoja na familia yake.
Septemba 8, mwaka huu, Liyumba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke alifikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga, akikabiliwa na kesi mpya ya kukutwa na simu gerezani.
Hata hivyo, baada ya kusomewa shtaka hili, alipewa dhamana akiwa amejidhamini kwa bondi ya sh 50,000 na kesi hiyo kuahirishwa hadi Septemba 29.
Desemba mwaka jana , Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi, alitupilia mbali rufaa iliyokatwa na Liyumba iliyokuwa ikiipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyomhukumu kwenda jela miaka miwili.
Hiyo ilikuwa ni baada ya kumtia hatiani kwa kosa moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo jaji huyo alisema anakubaliana na hukumu ya Kisutu kwani ilikuwa sahihi kisheria.
Mei 23, 2010, mahakimu wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, walitoa hukumu ya kumtia hatiani Liyumba kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma na hakimu mkazi mmoja Edson Mkasimongwa ambaye ndiye aliyekuwa akiliongoza jopo hilo kusikiliza kesi hiyo, alitofautiana na mahakimu hao wawili na akatoa hukumu ya peke yake ambayo ilimwachilia huru mshtakiwa huyo.
Hata hivyo, hukumu iliyotolewa na mahakimu hao wawili ndiyo ilibaki kuwa ni hukumu ya mahakama ya Kisutu na hukumu ya Hakimu Mkasimongwa ikabaki kwenye kumbukumbu za mahakama na haikutumika kwa ajili ya kumpatia adhabu Liyumba.