Kocha wa Taifa Stars Jan Poulsen.

MFANYABIASHARA na mwanamichezo maarufu nchini, Azim Dewji amesema kuwa, kamwe haafikiani na utetezi unaotolewa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah anayedai Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen hawezi kufukuzwa kwa sababu ana mkataba wa miaka miwili.

Dewji aliyewahi kuifadhili Simba na kuipa mafanikio makubwa Afrika, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, wadau wana nafasi kubwa katika ustawi wa soka ya Tanzania, hivyo wasipuuzwe kwa majibu ya juu juu. 

Alisema: “Nimesoma taarifa inayomnukuu Katibu Mkuu wa TFF kwamba Poulsen hawezi kutimuliwa kwa sababu ana mkataba wa miaka miwili, tena kwa sababu ya maoni ya wadau.

“Binafsi nasema hii si sahihi. Kocha anapimwa kwa vigezo vingi, lakini kama ameshindwa kazi na haoneshi dalili za kuelekea kufanikiwa, kwanini aendelee kuachwa kazini? Nahisi Angetile amepotoka na kamwe siafiki utetezi wake.”

Dewji aliongeza kuwa, kocha huyo raia wa Denmark alipaswa kuifanyia mapinduzi ya soka Stars, lakini anashangazwa kuona kila kukicha akifanya sawa na waliomtangulia, kuita kikosi kwa ajili ya mechi fulani huku akiwatumia wachezaji `wazee’ badala ya kuibua na kulea vipaji vipya kwa ustawi wa soka katika miaka ijayo.

“Hakuna jipya na wadau wanakata tamaa, ndiyo maana wanatoa ushauri kwa sababu wanaipenda timu yao.

Wakiendelea kukatishwa tamaa, nani atakwenda uwanjani na TFF itapata wapi fedha?

Ni vyema wakalitafakari hili, kwani tunashuhudia makocha wenye mikataba wakiachishwa kazi baada ya kushindwa kukata kiu ya waajiri wao,” alisema Dewji.



Osiah, jana alikaririwa na vyombo vya habari akimtetea Poulsen baada ya wadau mbalimbali wa michezo nchini kuhoji uhalali wa kocha huyo kuendelea kutafuna fedha za Watanzania, ilhali haoneshi mwelekeo wowote, zaidi ya kuporomosha kiwango cha wachezaji wa Taifa Stars.

Miongoni mwa wadau hao ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu aliyeonesha hofu ya Tanzania kutonufaika na lolote kutoka kwa kocha Poulsen.

Akizungumza na waandishi wa habari za michezo juzi, Osiah alisema: “Tunaheshimu maoni ya wadau wetu, akiwamo Mbunge Mangungu (Murtaza), ila lazima tuelewe kuwa Poulsen yupo kisheria na mkataba wake ni wa miaka miwili, hivyo hatuwezi kumuacha kwa mtindo wanaoutaka wao.

Poulsen aliyetua nchini kuirithi mikoba ya Mbrazil Marcio Maximo mwaka 2010, hajapata mafanikio makubwa akiwa na kikosi cha Stars, ukiondoa `ngekewa’ ya kutwaa Kombe la Challenge, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994.

Ilishinda kwa `matuta’ kuanzia hatua ya makundi hadi fainali. Na hata baada ya kuingia katika michuano ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012 na ile ya Kombe la Dunia mwaka 2014, Stars imeendelea kuwa ile ile ya kubahatisha uwanjani, hali inayompa wakati mgumu Poulsen aliyewabwaga wenzake watano katika mchujo wa mwisho wa kundi la makocha 59 waliokuwa wameomba kumrithi Maximo.