Nahodha alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya `Kunywa pombe kistaarabu' iliyoandaliwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Limited.
“Nitafuatilia taarifa za magari, nikiona ajali nyingi zinatokea katika mikoa yao, nitajua makamanda na wakuu wa usalama barabarani wameshindwa kazi,” alisema Nahodha.
Pia, aliwataka makamanda hao wa kila mkoa kuwanyang’anya leseni madereva wote watakaovunja sheria kwa kuendesha gari wakiwa wamelewa, jambo ambalo alisema linahatarisha maisha ya watu wengine wasiokuwa na hatia.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alisema kampeni hiyo yenye kauli mbiu “Rafiki hawezi kumuacha rafiki yake akanywa pombe na kuendesha gari,” itaongeza kasi katika kubadili tabia za watu wanaopenda kunywa pombe kupita kiasi.Kadhalika, alisema itapunguza madhara ya unywaji pombe.
“Unywaji pombe kupita kiasi ni suala la mtu binafsi lakini una madhara makubwa kwa watu wengine katika jamii, kwani kuna walemavu wengi na vifo vingi vinavyotokana na ajali za barabarani,” alisema Kamanda Mpinga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Teddy Mapunda, alisema kampeni hiyo itakuwa na ujumbe kupitia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa baa, mabango barabarani, vyombo vya habari, mafunzo kwa wanahabari na ujumbe katika kila vifaa vya matangazo.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments