Mdahalo uliowahusisha wagombea wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga kupitia vyama vya CCM, Chadema na CUF, juzi usiku ulitawaliwa na wafuasi wa vyama hivyo kutaka kuugeuza sehemu ya kampeni, hali iliyowalazimisha polisi kuingilia kati.
Polisi waliokuwa wamezingira eneo ka ukumbi wa mdahalo huo huku wakiwa na silaha mbalimbali za moto, walionya kuwa ikiwa wafuasi wa vyama hivyo wangeendelea na vitendo vya kutishia amani, mdahalo huo usingeendelea.
Mdahalo huo uliochukua saa mbili uliopewa jina la ‘Chagua Igunga tunayoitaka na Tanzania tunayoitaka’ uliwakutanisha wagombea na viongozi wa ngazi za juu wa vyama hivyo vyenye ushindani mkubwa katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.
Wakati wagombea hao, Dk. Peter Kafumu (CCM), Joseph Kashindye (Chadema) na Leopard Mahona (CUF), wakiingia ukumbini ndipo wafuasi wa vyama hivyo walipoamka na kuanza kutambiana nani ataibuka mshindi huku wengine wakinyanyua mabango yanayoonyesha picha za wagombea wao na kusogea mbele walipoketi wagombea wao. Wagombea hao wote walikuwa na walinzi waliosimama nyuma yao kwa muda wote wa mdahalo.
Hata hivyo, baada ya polisi kutoa onyo hilo, viongozi wa vyama hivyo walilazimika kwenda mbele ili kujaribu kuwasihi wafuasi wao watulie kwenye viti ili mdahalo huo uanze.
JULIUS MTATIRO
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema: “Iwapo watu watasimama na mabango na kuja mpaka hapa mbele hakuna kitakachoendelea, mimi binafsi nilitaka kuwasihi kuacha mambo hayo. Vyama vina discipline (nidhamu), wale watu wa CUF najua mnadispline tuonyeshe discipline tuwasikilize wagombea wafanye kazi yao.
ZITTO KABWE
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, naye aliingilia kati kutuliza vurugu hizo kwa kuamuru maofisa wa Chadema kumtoa nje mwanachama wake aliyekuwa akikaidi maelekezo.
“Wakati naanza kuongea watu walikuwa wametulia, akasimama mtu mmoja na bahati nzuri namfahamu ni wa Chadema na kwa kuonyesha discipline (nidhamu) namuagiza afisa usalama wa Chadema amtoe nje mara moja kwa sababu tuko hapa wagombea wetu wapate nafasi ya kueleza mawazo yao na hoja zao mbele ya wananchi, itasaidia sana tukiwa tumetulia, kelele hazitasaidia,” alisema.
NCHEMBA MWIGULU
Alipopewa nafasi ya kuwatuliza wanachama wake, Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM, Lameck Nchemba Mwigulu, alisema: “Baba ukienda kwenye harusi kama mwanao ana maadili huwa hatutoi sana nasaha, CCM utulivu ni jadi yetu.”
Baada ya hali kutulia, Mwenyekiti wa mdahao huo, Rosemary Mwakitwange, alianzisha mdahalo huo kwa kutupa maswali kwa wagombea hao ikiwemo ni vipi watalishughulikia tatizo sugu la afya na daraja la Mbutu ambalo limehusishwa na vifo vya akinamama na watoto?.
Akijibu swali hilo, Kashindye alisema: “Tatizo la afya linatokana na utekelezaji mbovu wa sera za CCM, zimetolewa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma za afya, lakini zikaliwa.

“Barabara ya Mbutu, mimi kama mweyeji hapa mwaka 2000 zilitolewa fedha sikumbuki ni milioni ngapi, (wafuasi wa CCM wakaanza kumzomea), hazikutumika, akaja aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa Sh. milioni 60 hazikutumika, Waziri Mkuu Mizengo Pinda akahidi hakuna chochote mpaka leo hakuna chochote kinachoendelea.”
Kwa upande wake, Mahona alisema kuwa huduma za afya katika jimbo hilo bado ziko chini na kwamba hadi sasa miaka 50 ya uhuru Igunga yenye idadi ya watu zaidi ya 180,000 ina vituo vya afya vinne na hospitali moja tu na hakuna magari ya kubebea wagonjwa.
Alisema katika wilaya nzima yapo magari mawili yanayosaidia katika utoaji wa huduma za afya na kwamba kwa ujumla suala la huduma za afya liko chini sana.
Mahona alikatishwa na vurugu ambazo zilisababisha mdahalo huo kusimama kwa muda ili kutoa nafasi ya kusuluhisha vurugu.
Hali hiyo iliwafanya polisi na Zitto kwenda kumchukua Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Aden Rage, aliyekuwa amekaa na baadhi ya wabunge wenzake pamoja na wana CCM akilumbana na wafuasi wa CUF kisha kumpeleka kwenye viti vya mbele ya ukumbi huo.
Mmoja wa askari polisi ambaye hakufahamika jina lake aliingilia kati vurugu hizo na kusema: “Ni rai yangu kama vurugu inatokea tuahirishe hili, lakini niwasihi wanachama tusikilize sera ndicho kilichotuleta hapa na ushabiki wa vyama tuuache, tunaomba amani itawale eneo hili na kwa yeyote atakayefanya vurugu tutamtoa nje.”
Baada ya hapo mdahalo huo uliendelea ingawa wakati mwingine wafuasi wa vyama hivyo vitatu vya siasa walishindwa kuzuia jazba zao na kuzomea wakati mwingine kushangilia kwa kuinua mabango ya wagombea wao.
Akijibu kuhusiana na daraja la Mbutu Mahona alisema: “Mimi naifahamu Igunga kijiji kwa kijiji ukweli ni kwamba daraja la Mbutu si pekee yake, ukweli ni kwamba yapo madaraja mengine manne lipo daraja lingine na mto Manonga, kule Choma watu wanakufa vile vile, kuna daraja la Nanga unapita unapoenda Mwabakatulu, Mpogolo nalo ni shida, kuna daraja la Utulia nalo ni shida.”
Kwa upande wake, Dk. Kafumu, alisema kuwa sera inayotekelezwa ni ya chama chao na akamshangaa mgombea wa CUF aliyesema kuwa akipewa ubunge atachukua siku 600 tu kulijenga daraja la Mbutu.
Kafumu alijitetea kuwa daraja hilo limeandikwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, ambayo imeainisha ujenzi wa daraja hilo.
“Kama mlisikiliza Bunge lililopita bajeti iliwekwa Shilingi bilioni tano na mkandarasi tayari alishapatikana kwa hiyo atakayeweza kujenga daraja la Mbutu si Mahona isipokuwa ni Chama cha Mapinduzi kwa ilani hii na msimamizi wake ambaye nitakuwa mimi.”
Kashindye: “Anadanganya mdahalo (Dk. Kafumu), kwa taarifa ya uhakika tangazo la tenda kwa ujenzi wa daraja la Mbutu limetoka mwezi huu wa tisa mwanzoni na zabuni zitakwenda kufunguliwa Oktoba, huyu mkandarasi anayesema amepatikana amemtoa wapi?”
Akijibu swali hilo, Dk. Kafumu alisema: “Nashukuru sana kwa hoja aliyoitoa inawezekana ulimi umeteleza (kelele), naomba mnisikilize, cha msingi hapa daraja la Mbutu lina fedha zimetengwa.”
Mwakitangwe alimrushia swali jingine Dk. Kafumu akimtaka aeleze nini kilimshinda akiwa jikoni (Kamishna wa Madini ), anadhani hivi sasa akiwa sebuleni atakiweza?”
Akijibu swali hilo, Kafumu, alisema hakuna kilichomshinda na kueleza kuwa akiwa Kamishna wa Madini alikuwa anashughulikia nchi nzima. “Sasa ninataka kuweka uwezo wangu wote katika Jimbo la Igunga.”
Mwakitwange aliwarushia swali lingine Kashindye na Mahona ambapo aliwahoji watawezaje kuifanya halmashauri ifanye kazi ipasavyo ikiwa madiwani wengi ni CCM?.
Mahona alisema ni kweli kumekuwa na wizi mkubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na kwamba fedha zimekuwa zikifika, lakini zinaliwa na serikali ya CCM.
“Kwa mfano, ngoja niseme kitu kimoja pale Simbo kulikuwa na Cluster (Kituo cha Walimu), wakati ule mimi nasoma sekondari mratibu wa hiyo Cluster alikuwa ni huyu (Kashindye), lakini baadaye ile Cluster ilitumia fedha nyingi sana lakini sijui nani alimpa promosheni ya kuwa mkaguzi wa shule,” alisema.
“Kwa sababu hadi hivi sasa ile Cluster hadi hivi sasa bado haijakabidhiwa, huyu hajakabidhi ofisi kwa miaka saba pale kuna upungufu wa saruji, kulikuwa na pikipiki haipo, mambo yote hayo unaweza kuona jinsi gani fedha zinaliwa….kwenye shule imekuwa ni shida, fedha zinaliwa. Ukienda kule Igombanilo shule ya msingi mkaguzi ni Kashindye… haiwezekani anapokea mshahara tarehe 30 halafu tarehe moja anasema yeye mpinzani, tunadanganyana hawa wanajuana.”
Akijibu swali hilo, Kashindye alisema kuwa kitendo cha kutumia fedha vema za ujenzi wa kituo cha elimu katika tarafa ya Simbo, ndicho kilichomfanya mwajiri wake kumpandisha cheo na kuwa Mkaguzi wa Elimu wa Wilaya ya Igunga.
“Huyu mwanafunzi wangu anajitahidi kunirushia madongo, huyu bwana wakati nafanya kazi pale yeye alikuwa anasoma hajui anachokisema (wanazomea ), ni kweli pale Simbo mimi nilikuwa ni mratibu wa kituo, tuliletewa Shilingi milioni 16.4 kwa ajili ya kujenga kile kituo,” alifafanua na kuongeza: “Mimi nilichokifanya pale nilifanya usimamizi makini, sikuwa na tamaa, tulijenga kile kituo, nyumba ya mwalimu tukapaka na rangi wakati hakikuwemo kwenye mpango na fedha milioni 1.8 zikabaki na kuanzisha jengo jingine ambalo halikuendelezwa hadi leo.”
Mmoja wa wapiga kura aliyejitambulisha kwa jina la Mkinga, alisema siku ya uzinduzi wa kampeni za CCM Dk. Kafumu, alisema kuwa ataendeleza yote yaliyoachwa na Rostam Aziz na kuhoji hataendeleza na ufisadi.
Akijibu swali hilo, Dk. Kafumu alisema ataendeleza yote aliyoanzisha Rostam kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya ya Igunga.
“Masuala mengine binafsi mimi sitaendeleza, ni kwa ajili ya wananchi wa Igunga yote hayo nitayaendeleza ndio kitu nilichosema, mambo hayo ni pamoja na ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2005 hadi 2010, lazima niyaendeleze,” alisema.
VIFAA KUWASILI KESHO
Katika hatua nyingine Msimamizi wa Uchaguzi huo, Protace Magayane, amesema maandalizi yake kwa kiasi kikubwa yamekamilika na kuwa vifaa ikiwemo fomu na karatasi za kupigia kura zinatarajiwa kuwasili kesho na kwamba kuwahi kwa vifaa hivyo kunatokana na umuhimu wake wa kuwaonyesha mawakala fomu wanazotakiwa kuzijaza.
VITUO 427 KUTUMIKA
Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake jana, Magayane alisema kuwa kutakuwa na vituo vya kupigia kura 427 na kwamba majina ya wapigakura yameshabandikwa katika vituo hivyo.
WATU 171,077 KUPIGA KURA
Kwa mujibu wa Magayane, watu 171,077 wameandikishwa katika orodha ya wapiga kura.
MAWAKALA KULA KIAPO LEO
Kuhusu mawakala wa vyama, alisema vyama vinavyowania ubunge kwenye uchaguzi huu vimeanza kuwasilisha majina ya mawakala wao ambao watakula kiapo cha kutunza siri leo.
“Vyama vimewasilisha majina ya wakala wao. Tunategemea waanze kula kiapo cha kutunza siri tarehe 27 ( leo) ,” alisema Magayane na kuongeza kuwa mawakala hao watapatiwa semina kesho na keshokutwa.
Alisema mawakala wanaotakiwa ni wale wanaoishi katika jimbo la Igunga waweze kuwatambua wapiga kura watakaofika vituoni.
Aliwataka wapiga kura kwenda kupiga kura Jumapili bila kuhofia usalama wao kwa kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika maeneo mbalimbali.
MALALAMIKO KUSHUGHULIKIWA
Kuhusu suala la malalamiko, Magayane, alisema amepokea malalamiko kutoka vyama vya Chadema na CCM na kwamba ameshawaandikia barua ya kutaka wapeleke maelezo.
Magayane alisema Chadema waliwasilisha malalamiko Septemba 24, mwaka huu wakidai kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage, alipanda jukwaani na bastola, kitendo ambacho ni kinyume cha maadili ya uchaguzi.
Alisema amewaandikia CCM kujibu malalamiko hayo na endapo watapatikana na hatia kwa mujibu wa maadili ya uchaguzi, watapewa onyo kali au faini ya Sh. 100,000 ama kuondolewa kwa mgombea wao katika uchaguzi.
Kwa upande wa CCM, Magayane, alisema alipokea malalamiko yao wakituhumu Chadema kuwarushia mawe na risasi.
Alisema amewaandikia barua Chadema kumpelekea maelezo yao kuhusiana na malalamiko hayo kabla ya kuwasilisha kwenye kikao cha maadili ya uchaguzi cha Jimbo la Igunga.
Alisema muda wa kuwataka kuwasilisha maelezo yao ambao ni saa 24, unamalizika leo.
TENDWA ATAKA UTULIVU
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji John Tendwa ameitaka Serikali, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi kuchukua hatua zote zilizo katika mamlaka yao ili kuhakikisha kwamba kipindi kilichosalia hadi ya siku ya kumchagua mbunge wa Jimbo la Igunga zinakuwa ni za amani na kwamba mbunge anapatikana katika uchaguzi ulio huru na wa haki.
Jaji Tendwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na NIPASHE kuhusiana na vurugu zinazoendelea katika kampeni za uchaguzi Igunga.
“Yanayoendelea Igunga yanatia aibu. Ni kama tuna eneo la Afghanistan ndani ya Tanzania. Kwa kweli hali imefika hapa kwa sababu ya kutowajibika ipasavyo kwa serikali, Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Jeshi la Polisi. Nasema hivi kwa sababu kama tungewajibika ipasavyo hali isingifikia hapa ilipo sasa,” alisema.
Alisema vitendo vya watu kumwagiwa tindikali, kushambuliwa kwa mkuu wa wilaya, watu kutembea na bastola hadharani na watu kurusha risasi na kuvunja magari ya watu ni ishara za wazi zinazoonyesha kuwepo kwa mapungufu ya uwajibikaji kimamlaka katika taasisi zilizo na majukumu ya kusimamia sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi.
Alifafanua kwamba mambo ya kumwagia watu tindikali, kutembea na silaha, kushambulia watu ni ya kijinai na kwamba kwa mji mdogo kama Igunga kwa mfano Jeshi la Polisi lilikuwa na kila sababu za kuchukua hatua stahili.
Hata hivyo, Tendwa alisema kwamba suala la mtafaruku unaoendelea Igunga atalipeleka kwenye kikao kijacho cha baraza la vyama vya siasa ili likajadiliwe kama mengineyo kwa kuwa hata vyama vyenyewe vina dhamana ya kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi tofauti na hali inayoendelea hivi
NEC YAVITAKA VYAMA KUHESHIMIANA
Nayo Nec imevitaka vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Igunga kufanya kampeni kwa kuheshimu maadili ya uchaguzi.
Kadhalika, Nec imemtaka msimamizi wa uchaguzi huo kutokukubali kutumiwa wala kushinikizwa na mtu yeyote ili atangaze matokeo ya uongo kwa kuwa akifanya hivyo adhabu yake ni kufungwa jela pamoja na kufilisiwa mali zake zote.
Kaimu Mwenyekiti wa Nec, Profesa Amon Chaligha, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema Nec imepata malalamiko mbalimbali katika kipindi cha kampeni yakiwemo ya watu kumwagiwa tindikali, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimaro, kudhalilishwa, watu kupanda jukwaani wakiwa na silaha pamoja na watu kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga.
Alitaja matukio mengine ambayo wameyapokea kuwa ni pamoja na watu kurushiana risasi za moto, kuharibu mali, kutumia lugha za matusi pamoja na wagombea kuhutubia mikutano ya kampeni kwa kutumia lugha za kikabila.
Alisema viongozi wa juu wa Nec kutoka jijini Dar es Salaam wamekwenda Igunga kuangalia hali ya kampeni na maandalizi ya uchaguzi huo.
Imeandikwa na Sharon Sauwa, Igunga; Richard Makore na Raphael Kibiriti, Dar.
CHANZO: NIPASHE