DAWA za kulevya ya aina mbalimbali ikiwemo bangi zaidi ya kilo tano, zimekamatwa zikiingizwa ndani ya Gereza Kuu la Arusha, imefahamika.
Kukamatwa kwa dawa hizo pamoja na mtu aliyekuwa akituhumiwa kujaribu kutenda uovu huo, kumethibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa.
Kaimu Kamanda alisema taarifa rasmi itatolewa leo. Habari za uhakika kutoka Gereza Kuu la Arusha zinasema kuwa mtu ambaye jina lake halijafahamika mara moja anayefanya biashara ya kuingiza dawa mbalimbali za kulevya gerezani ikiwemo bangi kwa malipo manono tofauti na bei ya uraiani, alikamatwa Jumatano iliyopita.
Mtuhumiwa huyo huingiza dawa hizo kupitia kwa wafungwa wanaokwenda kulima nje ya gereza hilo na kazi hiyo ya kuingiza dawa hizo hupewa kiranja wa genge ama mfungwa ambaye anakuwa anajua mchoro mzima wa askari siku hiyo ya uingizaji.
Vyanzo vya habari vilisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo haramu ni kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema wa ndani ya gereza hilo na nje waliotoa taarifa juu ya uingizaji uliokithiri wa dawa hizo.
Habari zilieleza kuwa baada ya askari kupata taarifa za uingizaji wa dawa hizo, waliweka mtego wa kumkamata mtuhumiwa huyo na ndipo siku hiyo alipokamatwa na kukutwa na kilo tano za bangi na ugoro kilo mbili.
Askari magereza walimkamata mtuhumiwa huyo na alikiri kufanya biashara hiyo mara kwa mara na katika kufanya uchunguzi zaidi, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kufungwa miaka 30 jela, lakini alitoka kwa rufaa ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari kutoka Polisi na Magereza, mtuhumiwa huyo alidai uingizaji wa dawa hizo hushirikisha askari magereza na wafungwa viranja.
Habari zaidi zilisema kuwa kufichuka kwa siri hiyo ni kutokana na “kutapeliana” kwa baadhi ya wahusika wa uingizaji wa biashara hiyo haramu ndani ya gereza.
Kamanda Mpwapwa alisema suala la kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo liko mikononi mwa Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa, Paul Leonard kwani halijamfikia, lakini hadi leo litakuwa mezani kwangu.

0 Comments