Yusuf Manji.

Mwanaharakati na mwanasheria maarufu nchini, Kainerugaba Msemakweli, amemjibu mfanyabiashara Yusufu Manji, akisema matusi, kejeli na vitisho alivyovitoa dhidi yake, kamwe haviwezi kumrudisha nyuma katika harakati zake za kuwafichua mafisadi.
Manji anadaiwa kutoa matusi, kejeli na vitisho hivyo, siku mbili baada ya Msemakweli, kuibuka na ushahidi wa kuipeleka mahakamani Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited inayotuhumiwa kukwapua Sh. bilioni 40 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Taarifa hiyo ya Manji ilishutumu na kukejeli elimu ya Msemakweli na kwamba, anatumiwa na kwamba, ushahidi wake alioupeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) umedhihirisha kwamba, ni muongo.

Msemakweli alisema baada ya kusoma na kuitafakari taarifa ya Manji dhidi yake iliyotolewa Septemba 8, mwaka huu, amebaini kwamba imejaa uongo na upotoshaji mwingi kiasi cha kumlazimu kuijibu.
“Haya yote siyo kweli na ni dhahiri kwamba Manji amepatwa na hasira na jazba baada ya kuumbuka,” alisema Msemakweli.
Kuhusu elimu, Msemakweli alisema Manji angetumia akili yake vizuri angegundua kwamba, yeye (Msemakweli) ana shahada ya sheria aliyotunukiwa mwaka 2008.
Kuhusu kutumiwa, alisema hakushangazwa na kauli hiyo, kwani wakati anaingia katika harakati hizo, alijua kuna watu wenye nia mbaya, ambao wangemtuhumu anatumiwa na kusema kuwa Manji mwa watu hao.
Kuhusu ushahidi wake kwa DPP, alisema anachokifanya Manji ni kutaka kuchezea akili za Watanzania, kwani ushahidi unaonyesha kuwa Kampuni yake ya Quality Finance Corporation Limited, iliisaidia Kagoda kikamilifu kufanikisha ukwapuaji wa fedha hizo EPA.
CHANZO: NIPASHE