Mahmoud Jibril waziri mkuu wa serikali ya mpito nchini Libya

Afisa wa Umoja wa Mataifa wa ngazi ya juu wa masuala ya kisiasa ameonya kuhusu hatari kutokana na silaha za kemikali nchini Libya.

Afisa huyo, Lyn Pascoe, alikuwa akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, uliohudhuriwa na waziri mkuu wa mpito wa Libya Mahmoud Jibril.

Bw Pascoe amesema mabadiliko ya haraka yanayofanyika nchini Libya yameongeza wasiwasi kuhusu usalama wa silaha za kemikali.

Amebainisha kwamba shughuli ya kuziteketeza silaha ilisitishwa mwezi Februari wakati harakati za mapinduzi zilipoanza na kundi la kimataifa la ukaguzi wa silaha lilipoondoka nchini humo.


Silah zikusanywe


Waziri mkuu wa mpito wa Libya Mahmoud Jibril ameelezea umuhimu wa silaha zilizotapakaa nchini humo kukusanywa haraka, siyo tu nchini Libya bali hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Lakini amesisitiza tena kwamba serikali yake haingeweza kutekeleza hilo au kukamilisha majukumu yake hadi hapo Umoja wa Mataifa utakapoziachilia mali zote za Libya zinazoshikiliwa tangu kuzuka kwa mgogoro nchini humo, wakati Muammar Gaddafi alipokuwa bado madarakani.

Mpaka sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelegeza baadhi tu ya vikwazo dhidi ya Libya.