Jeshi la Polisi nchini limeanzisha operesheni maalumu ya kukagua magari yanayosafirisha abiria kwenda sehemu mbalimbali nchini kufuatia ongezeko la ajali za barabarani.
Mkuu wa Operesheni wa jeshi hilo, Simon Sirro, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Sirro alikuwa akielezea hatua zinazochukuliwa na jeshi hilo baada ya ajali za barabarani kuongezeka nchini katika siku za karibuni.
Alisema operesheni watakazozifanya wakati huu zitajumuisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linalohusika na viwango na Wizara ya Ujenzi ambayo ndiyo yenye barabara.
“Ukaguzi wetu utalenga kuimarisha vituo vya ukaguzi kwenye maeneo mbalimbali ya barabara, kuendesha doria za pamoja zinazojumuisha maofisa toka idara mbalimbali za upelelezi, mbwa na farasi na usalama barabarani," alisema.

Kamanda Sirro alisema operesheni hiyo itakuwa endelevu na inalenga kuifikia mikakati iliyotolewa na Umoja wa Mataifa inayotaka kuhakikisha mambo matano yanafikiwa na kila nchi kwenye eneo la kupunguza ajali za barabarani.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na kuwa na barabara salama, magari salama, usimamizi wa sheria za barabarani, namna ya kuhudumia waathirika wa ajali za barabarani kuwa na watumiaji salama wa barabara.
Aliwaasa wananchi waelewe kuwa katika operesheni hiyo kutakuwa na ucheleweshaji wa safari kwa kuwa ukaguzi utafanyika kila siku kabla ya magari kuondoka toka kwenye vituo vya kuanzia na vituo vya ukaguzi njiani.
"Lakini nia ni kuhakikisha kwamba wanafika salama wanakokwenda," alisisitiza.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alisema jumla ya leseni bandia 215 zimekamatwa jijini Dar es Salaam.
Aidha, Kamanda Mpinga aliyekuwa ameambatana na Kamanda Sirro, alitangaza kuwa Wiki ya Usalama Barabarani itaanza Oktoba 3 hadi Oktoba 8, mwaka huu ambapo kitaifa itafanyika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.
CHANZO: NIPASHE