Wafanyakazi wawili wa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam wamehamishwa kutokana na tukio la Maiti 10 za vichanga kutoroshwa na kufukiwa katika shimo moja eneo la jirani na hospitali hiyo.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba, alisema wanafanya hao walihamishwa na kupelekwa katika hospitali za pembezoni.
Dk. Kamba alisema isingewezekana kuwafukuza wafanyakazi ikutokana na sheria kuwabana na ndio maana wamepewa adhabu hiyo.
Tukio hilo lilitokea Februari 2, mwaka huu ambapo maiti za vichanga hivyo zilifukuliwa kwenye shimo la takataka.
Kutokana na hali hiyo, tume iliundwa kwa ajili ya kuchunguza sakata hilo na kubaini kuwa vichanga hivyo havikuuawa wala vitendo vya kishirikina bali ubinafsi wa watumishi wa chumba cha kuhifadhia maiti kwa kuchukua fedha kutokakwa wafiwa kwa lengo la kwenda kuwazika. 
Ilibainika kuwa vichanga hivyo vilifariki wakati wa kuzaliwa au baada ya kuzaliwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, amesema hakuna kesi yoyote ya jinai kuhusiana na tukio hilo.
Wambura alisema jalada kuhusu tukio hilo lilipelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuchunguzwa kama kuna kesi au la.
Alisema tayari jalada hilo wamerudishiwa likiwa na maelekezo kuwa hakuna kosa la jinai.
Wambura alisema walielekezwa hatua za kinizamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wa Hospitali ya Mwananyamala ambao walihusika na sakata hilo.