Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mohammed Muya, alitangaza uamuzi huo wa serikali jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa waandishi wa habari na kusema kuwa unalenga kupunguza bei ya sukari kwa rejareja ambayo inazidi kupanda kwa kasi kubwa.
Muya alisema kuwa serikali itaanza kutoa vibali kuanzia sasa kwa wafanyabiashara wenye uwezo ili kuagiza sukari inayofikia tani 120,000 kutoka nje na kwamba mtu mmoja ataruhusiwa kuingiza shehena isiyozidi tani 5,000.
Alifafanua kuwa vibali hivyo vitatolewa na wizara yake na kwamba tayari wameunda kikosi kazi kwa ajili hiyo.
Hata hivyo, Muya alisema kuwa shehena hiyo ya sukari inatarajia kuanza kuingia nchini miezi miwili ijayo kuanzia sasa.
Alisema serikali imefanya utafiti wa bei ya sukari nje ya nchi na kubaini kwamba mfanyabiashara akiagiza bidhaa hiyo na kusamehewa ushuru, bei ya kilo moja inaweza kuuzwa kwa bei isiyozidi Sh.1,300 kwa kilo.
Muya alisema kuwa kwa sasa kilo moja ya sukari inauzwa kwa wastani wa Sh. 2,500 na kwamba serikali inataka kuhakikisha bei hiyo inapungua na kuwa chini ya hapo, lakini kwenye maduka na maeneo mbalimbali inauzwa kati ya Sh. 2,000 hadi Sh. 2,200.
Mapema mwaka huu serikali iliagiza wafanyabiashara kuuza kilo moja ya sukari isizidi Sh. 1,700 hata hivyo, agizo hilo lilipuuzwa.
Muya aliwaonya wafanyabiashara watakaokiuka masharti ya vibali walivyopewa kuingiza bidhaa hiyo bila kulipia ushuru kuwa watakabiliwa na adhabu ya kulipa faini ya Sh. milioni 30 au kifungo cha miaka mitano jela.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wengi wanavusha sukari kwa ajili ya kutafuta masoko ya bei ya juu. Nchini Kenya bidhaa hiyo inauzwa kwa Sh. 4,000 kwa kilo moja huku Uganda ikiuzwa Sh. 3,500.
Alifafanua kuwa mkakati wa serikali katika kumaliza tatizo la uhaba wa sukari ni kuongeza uzalishaji wake na kufikia kiwango kisichopungua tani 550,000.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania, Mathew Kombe, alisema mahitaji ya sukari nchini hivi sasa ni tani 380,000 wakati uzalishaji ni tani 300,000 kwa mwaka.
Kombe alisema kuwa mpango wa kuagiza sukari kutoka nje bila ushuru hautaathiri viwanda vya ndani badala yake alisema utasaidia kushusha bei ya sasa.
Alisema sukari ya nje inapoingia itaziba pengo la ubaha uliopo wa tani 80,000 bila kuathiri viwanda.
Alisema sababu kubwa ya kupanda kwa bidhaa hiyo ni kuongezeka kwa gharama za uendeshaji zikiwapo ongezeko la bei ya mafuta.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuzalisha sukari na viongozi wa Bodi ya Sukari.
Wakati serikali ikisema kuwa uagizaji wa sukari utasaidia kutatua upungufu wa bidhaa hiyo nchini, baadhi ya wazalishaji wa ndani wanalalamikia gharama za uzalishaji, kwamba unawalazimisha kupandisha bei ya bidhaa hiyo.
Katikati ya mwezi uliopita, bei ya sukari ilipanda katika mikoa yote nchini kutoka Sh. 1,800 hadi kufikia kati ya Sh. 2,200 na 2,500.
Agosti 25, Kiwanda cha sukari cha Moshi (TPC) kilitangaza kupandisha bei ya sukari kwa maelezo kuwa hali hiyo imetokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji.
Mkurugenzi wa TPC, Robert Baissac, alisema mfuko wa kilo 50 ulikuwa unauzwa kwa Sh. 75,050 na kuwa wasambazaji watauza kwa bei ambayo watapata faida.
“Sukari imepanda kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji…sisi hapa kiwandani sukari kwa mfuko wa kilo 50 inauzwa kwa bei ya Shilingi.75,050 na kwa mfuko wa kilo 25 inauzwa kwa Sh.37,530…pia kwa
mfuko wa kilo 20 tunauza kwa Shilingi 32,850, hizo ndizo bei zetu kwa hapa
kiwandani,” alisema.
Bei hizo ni wastani wa Sh. 1,500 kwa kilo, hivyo bei za rejareja mitaani zitakuwa ni juu ya hapo ili kufidia gharama za usafirishaji, kodi za serikali na faida katika biashara.
Baissac alisema kuwa viwanda vingine vya sukari katika nchi nyingine duniani ikiwemo Brazil vimepandisha bei ya sukari kutokana na gharama za
uzalishaji kupanda.
Tanzania imekuwa na utaratibu wa kusamehe ushuru wa sukari kila unapotokea upungufu, lakini pia ilipata kupatwa na sakata la vibali vya sukari wakati wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba, alipojipa jukumu la kutoa vibali hivyo.
Sakata hilo lilimfanya Simba kujiuzulu nafasi ya uwaziri baada ya uchunguzi wa tume iliyoundwa na Rais Benjamin Mkapa kubaini kuwa kulikuwa na ukiukaji wa taratibu katika utoaji wa vibali hivyo.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments