JINA la Sharobaro limejizolea umaarufu mkubwa hapa nchini, na kutumiwa na watu wengi kama sifa.
Kama ilivyokuwa kwa misemo mingine huwa na sababu, mpaka jamii kulipokea na kulikubali.
Mwanamuziki na mtayarishaji wa muziki wa kizazi kipya nchini, Raheem Rummy Nanji maarufu kama Bob Junior, Mr Chocolate au Rais wa Masharobaro,(Pichani juu) ndiye mwanzilishi na mmiliki wa Studio ya Sharobaro ambako ndiko jina hilo lilipoibukia.
Kama ilivyokuwa kwa watayarishaji wengine wa muziki, Rummy naye alipitia hatua mbalimbali za kujifunza muziki, kabla ya mafanikio.
“Kabla ya kujihusisha kutengeneza muziki, nilianza kuimba kipindi hicho nikiwa na Ali Kiba, Abby Skills na Mr Blue kabla hawajajulikana,” anasema.
Anaeleza kwamba muziki alitokea kuupenda kutoka kwa baba yake mdogo Guru Nanji ‘G- Love’ mmiliki wa Studio ya G Record. Anasema kipindi hicho studio hiyo ilikuwa maeneo ya Chang’ombe, yeye alikuwa akiishi na bibi yake Latifah eneo la Kariakoo.
Si hivyo tu, bali kipaji cha baba yake mzazi Rummy Nanji anayeishi Finland ambaye ni mwanamuziki wa Rock Star, kilichochea kipaji cha msanii huyo.
“Kwa kuwa baba mdogo ni mtayarishaji wa kazi za muziki, nami nikiwa karibu naye nikaanza kupenda kuimba, lakini pia nilipenda sana kusikiliza nyimbo za baba, ambazo zilinifanya nipende kuwa kama yeye,” alisema.
Anasema alipata wakati mgumu sana wakati anajifunza kuimba kwa kuwa walimchukulia kama anazuga na hakuna mtu aliyemkubali kwamba alikuwa na lengo la kweli kwenye muziki.
“Nilikuwa na wakati mgumu sana kwa kipindi hicho, kuwashawishi watu kwamba naweza kufanya muziki, watu wengi waliona nafanya muziki kwa kuwa baba yangu mdogo ndiye mwenye studio, lakini sikuwa nafanya kwa ajili ya undugu,” anasema.
Anasema baba yake mdogo ndiye mtu pekee aliyempa moyo wa kumtaka asikate tamaa na asonge mbele katika fani hiyo kwani siku moja angeweza kuwa msanii mkubwa.
“ Kwa kiasi fulani nilikuwa nimevunjika moyo, lakini mwaka 2005 nilitoa wimbo wa kwanza nikimshirikisha Mr Blue ulioitwa Blabla. Kwa bahati mbaya wimbo huo haukuweza kufanya vizuri.”
Wimbo huo haukuweza kufanya vizuri kabisa, mpaka 2007 mwishoni akatoa wimbo mwingine na Ali Kiba ambao uliitwa Nafsi Inateseka.
Anasema ingawa alikuwa akiimba, lakini pia muda mwingi aliutumia kwa kutengeneza muziki kwenye kompyuta yake ya nyumbani.
“Nyumbani nilikuwa na kompyuta, ambayo ilikuwa na programu ya kutengeneza muziki. Niliweza kuitumia kwa kutengeza muziki.
“Wakati naendelea kuimba nikajikuta muda mwingi nikijikita katika utengenezaji wa muziki.” Mwaka 2006 alikwenda Finland kumsalimia baba yake, na alipofika huko aliamua kuingia darasani kusomea muziki katika Chuo cha Music Power kwa muda wa miezi sita ambapo alitunukiwa cheti cha utengenezaji wa muziki.
“Kuhitimu mafunzo ya awali kulinitia moyo kidogo wa kufanya kazi kwa kiwango tofauti. Na hata baba yangu alifurahi sana, kwani alikuwa akiniunga mkono katika muziki.” Anasema baada ya kukamilisha kozi ya tasnia ya muziki, mwaka 2008 alirudi Dar es Salaam na baadaye kwenda kwa mama yake Khairun ambaye anaishi India.
“Unajua kile nilichokifanya Finland kilinipa morari sana na nikawa na kiu ya kutaka kujikita zaidi kwenye muziki, hivyo nilipofika India nikatafuta Chuo cha Magharadesh Music. Lengo langu lilikuwa ni kufanya kazi ya kimataifa zaidi, hivyo kila nilipokuwa nikienda nilikuwa nasomea muziki ili kuongeza ujuzi,” anasema.
Anaongeza: “Nilijifunza kwa muda wa miezi sita. Jambo kubwa nililokuwa nikifanya kila nilikokwenda ni kuhakikisha nanunua kifaa kimoja cha muziki. Lakini pia wazazi wangu waliweza kuninunulia vifaa kama kompyuta, mixer, mic, kinanda na vingine vya muziki na walinisaidia sana kukamilishia vifaa vya kutengenezea muziki.”
Anasema alipofika Dar es Salaam mara moja alianza kujikita katika kutengeneza muziki, huku akitafuta jina la studio, “ Haikuwa rahisi kupata jina, nilipata kwa tabu sana huku nikikatakata majina tofauti, majina yangu, ya familia na kuunganisha mpaka lilipotokea neno Sharobaro.
“Jina hili lilinijia akilini wakati nikijaribu kutafuta jina la studio. Nikaamua kuipa studio yangu jina hilo na mimi kujiita kwa jina hilo nikiwa kama kiongozi.”
Raheem anasema: “ Kwa mara ya kwanza mwaka 2009, nilitengeneza wimbo wa ‘She is Sex’ wa mwanamuzki Tox Star, aliomshirikisha Ali Kiba.
Ambao ulipigwa sana redioni na kuoneshwa kwenye luninga.” Anasema kukubalika kwa kazi hiyo kulimpa motisha ya kuendelea kutengeneza kazi za wasanii wengine kwa kutoa nafasi kwa wasanii wanaoweza kuimba hususani wale chipukizi na kuwa chini ya lebo yake ya Sharobaro kwa ajili ya kufanya kazi bure wakiwa chini yake.
Raheem anasema nafasi hiyo ilimfanya kutoa wimbo wa Nasir Abdul ‘Diamond’ uliojulikana kwa jina la ‘Mbagala’ mwaka 2010.
“Wimbo wa Mbagala ndio ulinitambulisha vizuri kwenye medani ya muziki wa kizazi kipya, na hapo jina la Sharobaro sasa likaanza kuwa gumzo masikioni mwa kila mmoja, hii ilionesha kukua kwa studio yangu na kazi yangu pia.” “Nilifyatua vibao vingine, kama Lofa wa Top C ambavyo vilizidi kunipaisha kwenye tasnia ya muziki.”
Raheem anasema, baada ya hapo akawa anasaidia kukua kwa muziki wa kizazi kipya bila ya kuangalia maslahi gani anayopata. “Nilisaidia wasanii kutunga nyimbo, wengine nimewapa mawazo ya kutengeneza muziki, na wengine nimewafunza walikuja hawajui. Wengi niliwafundisha jinsi ya kuimba kwenye mstari wa biti na kuwapa melodi ya kuimbia.” Anazitaja baadhi ya nyimbo ambazo alisaidia kuzitunga na kushiriki kuziweka sawa kwa njia moja au nyingine kuwa ni kama ‘Muhogo Kiazi’ wa Nuru, ‘Naumia na Roho’ wa Lady Jaydee na Mr Blue.
Anasema baada ya kutengeneza kazi hizo, aliona ni wakati wa yeye pia kuonesha kipaji chake na kuimba wimbo wa ‘Oyoyo’ ambao ulimuongezea umaarufu, pamoja na kuinua zaidi jina la Sharobaro. “ Hadi sasa nimeshakamilisha albamu yangu ya kwanza inayoitwa Oyoyo yenye nyimbo kumi na mbili.”
Anapozungumzia wasanii wanaomvutia katika medani ya muziki anawataja Fally Pupa na Nice Lucas Mkenda ‘Mr Nice’ ambao ndio wanaomfanya yeye aweze kuimba na kucheza pia. Anasema kuwa pamoja na kiu yake kupenda kufanya kazi na baba yake ikiwa ni kumtengenezea midundo, lakini pia anapenda kufanya kazi na baadhi ya wasanii wa Afrika Mashariki kama Wyre na Radio ‘Goodlife’ wa Uganda.
Aidha, Raheem anaamini kuwa wasanii wengi wanajua muziki ila kinachowakwamisha ni ukosefu wa fedha za kuwatoa hatua moja na kwenda nyingine katika mafanikio.
“Fedha ni tatizo kubwa hususani kwa wale wanaotaka kuchipukia katika fani hii, nalijua hili kwani nimetokea huko, na ndiyo maana nikaanzisha kundi la Sharobaro ili kusaidia wasanii ambao wanaweza, lakini wamekosa nafasi.”
Raheem ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia yao na kufuatiwa na Ali Rummy Nanji amezaliwa jijini Dar es Salaam 1989, na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Olimpio mwaka 2006, na baadaye elimu ya sekondari katika Shule ya St Mary’s.
“Nilitaka kusomea kozi ya mawasiliano lakini sikuweza kupata kutokana na kukosa sifa.” Anasema lengo lake ni kuhakikisha kuwa Kampuni ya Sharobaro inakuwa kampuni kubwa itakayokuwa ikitengeneza muziki na video zenye kukidhi viwango vya kimataifa. “Maisha yangu kwa sasa nimeyaweka kwenye muziki, na mara chache nimekuwa nikijihusisha pia na fani ya uigizaji baada ya kuigiza filamu kadhaa pale ninapohitajika kama Candly ya Jack Wolper. Pia nimekuwa nikijihusisha kutengeneza matangazo, na utangazaji ikiwemo kwenye kipindi cha Bongo Star Search Second Chance 2011.”
Raheem ambaye kwa sasa anamiliki nyumba, gari na kiwanja, anajipanga kukamilisha albamu yake ya pili.Anasema akifikisha miaka 40, ataachana na masuala ya muziki na kujikita katika biashara ya kimataifa ambayo anasema ataifikiria baadaye.
0 Comments