Mlinzi wa Manchester United Patrice Evra amemueleza meneja wake Sir Alex Ferguson anahitaji kufuatilia tuhuma dhidi yake za maneno ya kibaguzi zilizotolewa na mshambuliaji wa Liverpool Luis Suarez.
Evra alitoa tuhuma hizo baada ya timu hizo mbili kwenda sare ya bao 1-1 katika uwanja wa Anfield siku ya Jumamosi.

Ingawa mlinzi huyo wa kushoto anaamini ushahidi uliorekodiwa katika televisheni utatoa haki kutokana na madai yake, Suarez amekanusha tuhuma hizo na kusema "amehuzunishwa" na madai hayo.

"Nimezungumza na Patrice. Ana nia ya kufuatilia suala hilo", alisema Ferguson.

Utata huo ulitokea mwishoni mwa mchezo ambao huwa haukosi vijambo zinapokutana timu hizo.

Kabla ya mchezo huo uliochezwa siku ya Jumamosi mchana, meneja wa Manchester United aliwataka mashabiki wao kutosimama wakati wa mechi hiyo na kuwataka mashabiki wa pande zote mbili kujizuia kutoleana maneno ya kashfa hasa kuhusiana ajali ya ndege ya Munich na Hillsborough.

"Si jambo rahisi kwetu," alisema Ferguson. "Kila mtu anafahamu Manchester United na Liverpool wanajukumu kubwa hasa kutokana na yale yanayotokea uwanjani.

"Jumamosi ilikuwa ya ajabu sana. Mashabiki wa timu zote walikuwa na nidhamu. Hakukuwa na nyimbo zozote za kukashifiana kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Mashabiki wote wanastahili kupongezwa kwa yote hayo.

"Si jambo ambalo tunataka kulihusisha na Liverpool na si dhidi ya Liverpool.

"Kusema kweli Patrice anahisi anasumbuliwa na yale yaliyosemwa dhidi yake. Suala hilo kwa sasa lipo mikononi mwa FA."