NGULI wa zamani wa soka wa Liberia, George Opong Weah ambaye kwa sasa amejikita katika
siasa na biashara, ametimiza kiu yake ya muda mrefu ya kuitwa msomi, baada ya hivi
karibuni kutunukiwa Shahada ya Utawala wa Biashara.
Ametunukiwa Shahada hiyo katika Chuo Kikuu cha DeVry kilichopo Florida, Marekani
alikokuwa amejichimbia darasani kwa zaidi ya miaka miwili.
“Ilikuwa ndoto yangu kukaa darasani na kusoma. Namshukuru Mungu nimetimiza ndoto yangu nami kwa sasa ni miongoni mwa wasomi wa kweli,” alisema Weah, kijana mwenye umri wa miaka 45 ambaye kauli yake inatafsiriwa kuwa inajibu mapigo ya watu waliombeza wakati anawania urais wa Liberia kwa tiketi ya Congress for Democratic Change Party (CDC) mwaka 2005.
Wakati anawania urais mbele ya msomi aliyekuja kuibuka mshindi katika uchaguzi huo,
Ellen Johnson-Sirleaf, wengi hasa wa vyama vya upinzani walimbeza, wakidai hawawezi
kuongozwa na mtu asiye na upeo mpana, kwa maana ya msomi.
Mithili ya mwiba, maneno hayo yalimchoma Weah, ndiyo maana akaamua kujipanga upya
na kurudi darasani. Hata hivyo anasisitiza kuwa, hakurudi kusoma kwa ajili ya kuusaka urais, bali kuonesha kuwa, hakushindwa kusoma kwa sababu ya kutokuwa na `kitu’ kichwani.
“Wote tunakuwa na ndoto za kusoma mpaka Chuo Kikuu. Baadhi wanaweza, wengine waliikosa
kabisa hiyo nafasi na wengine walisubiri hadi wakati mwafaka.
Kwa upande wangu, nilisoma kwa njia ya masafa marefu, lakini haikusaidia sana, ndipo baada ya kustaafu nimekaa darasani na kufanikiwa kupata digrii ya kweli. Nashukuru imewafurahisha wazazi wangu, familia yangu na pia kuwaziba midomo walionibeza kwa kutokuwa na digrii,” anasema.
Anaongeza kuwa, ingawa kwa upande wake ametimiza ndoto ya kielimu, anasema hilo ni funzo
kwa watu wengine kwamba, elimu haina umri na wala haina mwisho. Anawageukia wapinzani
wake waliombeza kwa kutosoma akiwaambia kuwa, uongozi kamwe hauhitaji shahada za
chuo kikuu, bali busara na uelewa wa mambo na pia kukubalika kwa wananchi.
“Kuna wengi walioongoza vizuri hata bila ya kuwa na digrii, bali kwa sababu
wameaminiwa na wao hufanya kazi usiku na mchana ili kutowaangusha waliomwamini. Na
hata kwa Waliberia, ni zamu yao kuamua kama nafaa kuwaongoza au hapana, lakini elimu isiwe kigezo pekee.
“Ila ninajifahamu kuwa nina kipaji cha uongozi, ninachosubiri ni maamuzi ya Waliberia,
lakini naamini ipo siku nitakuwa Rais wa nchi yangu,” anasema Weah amejiengua kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na badala yake akimpisha Balozi Winston Tubman kuwania urais kwa tiketi ya CDC akichuana na Sirleaf, huku yeye akiwa mgombea mwenza wa Tubman.
Anasema Tubman ana uzoefu wa uongozi na ana nafasi kubwa ya kuwaunganisha Waliberia.
Hata hivyo, watabiri wa mambo wanabashiri kuwa Tubman atakuwa na kibarua kigumu
mbele ya mwanamama Sirleaf, msomi na mchumi wa miaka mingi ambaye wiki iliyopita nyota
yake iling’ara kwa kuwa mmoja wa washindi watatu wa tuzo ya Nobel kwa mwaka 2011.
Kwa Sirleaf mwenye umri wa miaka 73, tuzo hiyo ina maana kubwa, kwani imemwongezea
heshima na hivyo kuaminika huenda akashinda uchaguzi uliofanyika na matokeo ya mwisho kutarajiwa kutolewa kati ya sasa na Oktoba 26 mwaka huu na kama atashinda, ataendelea
kuwa rekodi barani Afrika.
Anashikilia rekodi ya kuwa Rais wa Kwanza mwanamke kuwahi kuchaguliwa barani Afrika.
Pamoja na rekodi hiyo na tuzo ya hivi karibuni, Weah anasema: “Sikugombea urais, lakini
nimeshiriki kikamilifu katika kampeni kama mgombea mwenza.
Miongoni mwa vitu nilivyojifunza shule, katika darasa langu la watu 303 tuliosoma biashara, wakati mwingine unaweza kuwa na maamuzi, lakini nimeamua kutumia mbinu mbadala.
“Mimi ni baba wa CDC, lakini cha msingi ni kwamba mwisho wa siku tunataka CDC ichukue
nchi, hivyo si vibaya kumpa nafasi mtu mwenye uwezo, uzoefu na anayekubalika kote
Liberia, na kwa wakati huu, nadhani Winston Tubman ndiye chaguo sahihi la Waliberia.”
Anaongeza kuwa, katika kuthibitisha kuwa hakubahatisha kupata Shahada ya kwanza, baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu anakusudia kuanza masomo ya Shahada ya Uzamili (digrii ya pili) kwa kusoma darasani, huku akitamba kuwa, atamaliza na kufaulu vizuri.
Je, Weah ni nani hasa? Huyu ni mwanasoka mahiri kuwahi kutokea katika Bara la Afrika, akiwa
na rekodi ya kipekee. Weah, aliyevuna utajiri mkubwa wa fedha katika soka, ndiye Mwafrika pekee kuwahi kutwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia.
Aliiweka rekodi hiyo mwaka 1995, mwaka ambao aling’ara na kutwaa pia Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Ulaya na pia Mwanasoka Bora wa Afrika. Kisoka, nyota huyo aliyezaliwa Oktoba mosi mwaka 1966 katika kitongoji wanachoishi watu wenye maisha duni cha Clara, jijini Monrovia, alianzia katika klabu Invincible Eleven na baadaye Tonnerre Yaounde ya Cameroon.
Licha ya kucheza soka, alikuwa pia tayari mwajiriwa wa Shirika la Mawasiliano la Liberia
alikokuwa ameajiriwa kwa nafasi ya fundi wa simu.
Mambo yalimnyookea mwaka 1988 baada ya kujikuta akinyakuliwa na Monaco ya Ufaransa alikofanya mambo makubwa kabla ya kutua Paris Saint Germain (PSG), klabu nyingine ya Ufaransa aliyoichezea kati ya mwaka 1992 na 1995.
Makali yake uwanjani yalimpeleka AC Milan ya Italia mwaka 1995. Nako aling’ara hadi
mwaka 2000 alipotua England kuichezea Chelsea na baadaye Manchester City. Hata hivyo
mwaka 2001 alirejea Ufaransa kuichezea Marseille na kuamua kwenda kustaafia soka Falme za
Kiarabu katika klabu ya Al Jazira.
Ndipo baada ya kustaafu, alijikita katika shughuli za kijamii na kujikuta akiangukia katika
siasa, akiwania Urais wa Liberia mwaka 2005. Je, baada ya kuzidiwa kete na mwanamama wa shoka Ellen Johnson Sirleaf mwaka 2005, Weah ataweza kuingia Ikulu kwa mlango wa nyuma akitumia mgongo wa Tubman?
Kura ndiyo kwanza zimeanza kuhesabika na katika siasa lolote linawezekana, hata hivyo hilo ni
jambo la kusubiri. Huyo ndiye George Opong Weah ambaye kwa kiasi kikubwa amelelewa na bibi yake mzaa baba, Emma Klonjlaleh Brown, huku kwa zaidi ya miaka kumi mwanasoka huyo akiwa muumini wa dini ya Kiislamu, kabla ya baadaye kurejea katika Ukristo.
Ni baba wa watoto wanne aliozaa na mkewe mwenye asili ya Jamaica, Clar. Watoto wao ni
George Jr, Martha, Timothy George na Jessica. George Jr amefuata nyayo za baba yake, kwani kwa sasa anaichezea FC Baden ya Uswisi na timu ya vijana ya Taifa ya Marekani akiwa na swahiba wake Freddy Adu. Aliwahi kuichezea pia AC Milan ya Italia.
0 Comments