Mahakama moja mjini Nairobi imemfunga maisha mtu aliyekiri kuwa mfuasi wa al shabaab na aliyetekeleza shambulizi la gureneti kwenye kituo cha mabasi mapema wiki hii.

Elgiva Bwire Oliacha alia Mohammed Seif(pichani juu) alikiri kusababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine 20 baada ya kuwarushia guruneti.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu mkaazi Grace Macharia, alisema mahakama imeridhika kuwa alipanga kuwaua watu wengi na lazima apewe adabu kali.

"Ili iwefunzo kwa watu wengine wenye nia kama yako, mahakama imeona vyema itoe kifungo hicho cha maisha kuwazuia kupanga harakati kama zako" alisema Hakimu Macharia.

Bw Bwire pia atatumikia kifungo cha miaka 15 kwa kuwa mwanachama wa kundi la al -shabaab ambalo limepigwa marufuku nchini Kenya na miaka mengine 7 kwa kupatikana na silaha bila kibali.


Licha ya hukumu hiyo kali, kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 alionyesha kutogutushwa na kuwaelezea waandishi wa habari kuwa amefurahi na wala hatakata rufaa licha ya kupewa fursa hiyo.

Bwire, inasemekana alipata mafunzo ya kijeshi chini ya makamanda wa al-shabaab kuanzia mwaka wa 2009 mjini Mogadishu.

Awali, washukiwa wengine wawili wanaoaminika kuwa walishirikiana naye kutekeleza shambulio hilo mjini Nairobi pia walifikishwa mahakamani.

Hata hivyo, Omar Muchiri Athman alias Hussein na Stephen Macharia alias Mchangoo walikanusha madai hayo na wamezuiliwa rumande hadi tarehe 4 mwezi ujao.