Mkuu wa Shule achomwa moto Igunga

*Adaiwa kuiba saruji ya shule

Na Mwandishi Wetu, Igunga

MKUU wa Shule ya Sekondari ya Mwashiku, Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora, Bw. Charles Medadi (42) amepigwa hadi kufa kisha mwili wake kuchomwa moto na wananchi
wenye hasira baada ya kukamatwa akiwa na mifuko minane ya saruji za shule hiyo.

Habari kutoka eneo la tukio zilidaiwa kuwa marehemu alikamatwa na wananchi akiwa na saruji hiyo huku akidaiwa kujiandaa kwenda kuiuza.

"Nilipofika, wananchi walisema Mwalimu huyo alikamatwa akijiandaa kuuza hiyo simenti (saruji). Kumekuwa na malalamiko kuwa vifaa vya ujenzi na fedha shule hiyo vinaibwa na kutumika vibaya, walikuwa wanafuatilia," alisema mtoa habari wetu kutoka eneo la tukio.

Polisi wilayani Igunga ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa taarifa zaidi itatolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Bw. Antony Rutta kama utaratibu wa jeshi hilo unavyoelekeza.

Wakati tunakwenda mtamboni gari la polisi yenye namba PT 1825 ikiwa na askari saba wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya ya Igunga, Bw. William Mlekwa, iliwasili mjini hapa ikiwa na mwili wa marehemu huku ukiwa umeungua vibaya.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga. Wakati huo huo Bw. Bathlomeo Charles, (28) mkazi wa Igunga mjini amekatwa mapanga wakati akitoka dukani kwake mjini hapa.

Tukio hilo lilitokea saa 5 usiku wa kuamkia jana eneo la Posta muda mfupi baada ya kufunga dukani lake na kuelekea nyumbani ndipo walipoibuka kundi la watu na kumwamuru kutoa fedha.

Akizungumza kwa taabu akiwa wodi namba 8 katika hospitali ya Wilaya ya Igunga alikolazwa Bw. Charles alisema baada ya kukataa kutii amri ya kutoa fedha watu ahao walianza kumshambuliwa na kumkata kichwani na mkono wa kushoto ambao ulibaki ukining'inia.

Polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba Kamanda Rutta anatarajiwa kulitolea ufafanuzi zaidi baada ya uchunguzi kukamilika