Vikosi vitiifu kwa serikali ya mpito ya Libya vimeanzisha mashambulizi makali katika mji wa Sirte ikiwa ni moja ya ngome za mwisho za Kanali Gaddafi.

Mamia ya magari yameelekea katika mji huo kutoka mashariki na magharibi na sasa yamekaribia katikati ya mji.
Maelfu ya raia wameondoka Sirte lakini wengi zaidi wamesalia huko.

Mwandishi wa BBC aliye katika vitongoji vya mji huo, anasema haya ndio mashambulizi makubwa zaidi kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni.

Mfululizo wa mashambulizi ya vifaru na makombora umelenga mji huo wa Sirte na moshi mwingi umeonekana kufuka mjini humo karibu kilomita 360 mashariki mwa Tripoli ambapo majengo mengi yamebomolewa na mengine kuteketezwa.


Hii inaonekuwa kuwa hatua ya mwisho ya kuuteka mji huu alikotoka Kanali Gaddaffi. Libya imeshindwa kufanya mipango yake kwa kuwa bado mji huo haujakamatwa.

Vikosi vya serikali ya mpito vinatoka Misrata upande wa magharibi na Benghazi upande wa Mashariki.

Vikosi vya Benghazi vimefika karibu kilomita moja kuingia katika ya mji huo lakini vimekabiliwa na pingamizi kubwa kutoka kwa walenga shabaha walio ndani ya mji huo.

Vikosi vya NTC vimewapa wakazi wa Sirte fursa ya kuondoka kutoka mji huo lakini kuna hofu kuwa maelfu wameshindwa kufanya hivyo, inaaminiwa labda huenda walesikiza na kuamini onyo inayotolewa na wapiganaji wa Gaddafi kuwa watashambuliwa na vikosi hivyo vya serikali ikiwa watajisalimisha.

Juhudi za kufanya mashauri na makamanda kutoka pande zote zimekosa kufaulu.