Amri ya kutotoka nje imetolewa mjini Cairo kufuatia machafuko yaliyotokea wakati a maandamano yaliyofanywa na wakristo wa dhehebu la Coptic, nchini Misri.
Takriban wati ishirini na nne wameuawa na zaidi ya mia mbili wamejeruhiwa vibaya katika machafuko mabaya zaidi ya kidini kuwahi kutokea nchini humo.
Wakristo hao walikabiliana na wanajeshi waliowalaani kwa kutowalinda dhidi ya mashambulio yanayotekelezwa na baadhi ya makundi ya kiislamu yalio na misimamo mikali.

Wanajeshi wamekuwa washika doria katika sehemu mbali mbali katikati ya jiji katika juhudi za kutuliza hali.

Waziri mkuu Essam Sharaf amewasihi raia wote wadumishe umoja katika hotuba iliotangazwa moja kwa mnoja kuptia televisheni ya taifa.

Maandamano hayo ya jumpili, yalipangwa na wakristo wa dhehebu la coptic baada ya kanisa lao mmoja karibu na Aswan kuteketezwa wiki iliopita.

Wafuasi wa dhehebu hilo walilaani utawala wa kijeshi nchini misri wakisema kuwa ulikuwa unafungia jicho mashambilizi dhidi yao yanayotekelezwa na waislamu wenye misimamo mikali.

Magari ya jeshi yaliteketezwa na kupigwa na mawe wakati wa makabiliano hayo. Nazo risasi zimesikika hewani na wanajeshi wametumia gesi za kutoa machozi kutawanya waandamanaji hao.

Makabiliano kati ya makundi ya kidini nchini Misri yamekuwepo kabla kuondolewa kwa utawala wa Rais Hosni Mubarak, lakini dalili zinaonyesha kuwa huenda yanazidi.

Wakristo ambao ni asilimia kumi ya jumla ya idadi ya watu nchini humo wanasema kuwa harakati za waislamu wenye msimamo mikali zinawatia hofu.

Na huku uchaguzi wa ubunge ukitarajiwa mwezi ujao, utawala wa mpito unajaribu kuhakikishia kila kundi kuwa sauti zao zitasikizwa.