KATI ya madereva 8,165 wa pikipiki zinazosafirisha abiria ndani ya Jiji la Dar es Salaam, 504 pekee ndio wenye leseni za udereva wa vyombo hivyo vya moto.
Hali hiyo imeelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ajali za barabarani hasa zinazosababishwa na pikipiki maarufu kama bodaboda kwa kuwa wengi wanaoziendesha hawana ujuzi wa udereva wala kujua sheria za usalama barabarani.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Serikali ya APEC inayowasimamia madereva wa pikipiki wa Dar es Salaam ambayo pia hushughulika na kuondoa umasikini na utunzaji wa mazingira, Respicius Kumanya, Kamati ya Usalama Barabarani ya Mkoa haina budi kuhakikisha idadi ya wenye leseni inaongezeka ili kupunguza ajali.
Kumanya alisema hayo katika uzinduzi wa Wiki ya Usalama Barabarani, Dar es Salaam na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) nchini, Tim Clarke.
Alisema APEC kwa kujua umuhimu wa mafunzo kwa madereva wa pikipiki, imejitahidi kwa uwezo wake kutoa elimu ya udereva na hivyo kuwezesha kupungua kwa ajali za mara kwa mara ingawa ni kwa kiasi kidogo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki alisema wananchi hawana budi kuwakemea madereva wa daladala wanaokataa kuwabeba wanafunzi kwa kuwa kitendo hicho ni unyanyasaji.
Pamoja na kusisitiza uendeshaji makini wa vyombo vya moto na vyote vinavyotumia barabara nchini ikiwemo kuzingatiwa kwa sheria za usalama barabarani, anataka wananchi
wasiwaonee haya madereva na makondakta wanaofanya unyanyasaji huo kwani wanakosea
kisheria.
Naye Balozi Clarke aliipongeza Serikali kwa kubuni mbinu mbalimbali za kupunguza ajali na kusema ingawa takwimu za ajali na vifo vya vinavyotokana na vyombo vya moto zinatisha,
wanatambua jitihada zinazofanyika kuzizuia.
0 Comments