WATANZANIA 25 wamefukuzwa nchini Kenya tangu kuanza kwa mwaka huu baada ya kumaliza kutumikia vifungo kutokana na makosa mbalimbali ya kiuhamiaji yakiwemo ya kuishi nchini humo bila kuwa na vibali.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Uhamiaji Mfawidhi, Frederick Kiondo wa kituo cha uhamiaji cha Holili-Himo mkoani Kilimanjaro wakati akimweleza Mkuu wa Mkoa huo taarifa fupi ya namna kituo hicho kinavyofanya kazi.
Kiondo alisema licha ya Watanzania hao kufukuzwa nchini humo pia kuna wageni kutoka nje ya nchi waliokataliwa kuingia nchini Tanzania kwa kipindi hicho hicho cha mwaka 2011 kwa sababu mbalimbali.
Alisema kati yao, wapo Wakenya wanane wenye asili ya Somalia ambao walizuiliwa kuingia nchini kutokana na kutokujua lugha ya Kiswahili wala Kiingereza.
Aliongeza kuwa, walizuiliwa Waethiopia watano kutokana na kutokuwa na viza rejea, Wabangladeshi wanane pia kutokuwa na viza rejea na Mwingereza mmoja aliyeshindwa kulipa viza.
Aidha, Kiondo aliongeza kuwa kwa mwaka huu tayari kituo hicho kimetoa viza 327 zenye jumla ya dola za Marekani 17,610 (Sh milioni 28) na matarajio ya kituo hicho kufikia Desemba ni kulipisha viza 198 za dola 9,900 (Sh milioni 15.8) hivyo kufanya viza zitakazokuwa zimetolewa kwa mwaka huu kufikia 525 zenye thamani ya dola za Marekani 27,510 (Sh milioni 44).
“Viza moja ya kawaida ina thamani ya dola za Marekani 50 (Sh 80,000), tumeboresha huduma zetu kwa wateja ili kutoa ushawishi na mvuto kwa wageni wengi wapitie hapa kuingia nchini na kulipa viza ili pato la taifa liongezeke,” alisema Kiondo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliwapongeza wafanyakazi wa kituo hicho na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa kwani wao ni taswira ya taifa kwa wageni wangiao nchini.
“Nyie ndiyo mnaotuwakilisha maana mko hapa mpakani kwa hivyo mgeni akifika hapa akiona ukarimu wenu atapata picha ya Watanzania wote, fanyeni kazi kwa moyo wa uzalendo, wakirimuni wageni, epukeni kabisa vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki.”http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=21800
0 Comments