Kwa mujibu wa mkuu wa shirika la kitaifa la mafuta nchini Libya, nchi hiyo inatarajiwa kurejesha uzalishaji wa mafuta ambayo hayajasafishwa katika kiwango cha awali kabla ya vita ikiwa ni mapipa milioni 1.6 kwa siku kufikia mwaka 2012.
Nuri Berouin amesema kiwango cha uzalishaji mafuta hayo kimefikia sasa mapipa 600,000 na kinatarajiwa kuongezeka kwa mapipa mengine 200,000 kwa siku kufikia mwisho wa mwaka huu.
Alisema kuwa kukarabatiwa kwa miundombinu ya sekta ya mafuta kutagharimu mamilioni ya dola.
Bw. Berouin amekuwa akizungumza katika kikao cha kiuchumi cha wanunuzi wa gesi kinachofanyika Qatar.
"Uzalishaji wetu umefikia mapima 600,000 ambayo kati yake mapipa 140,000 hupelekwa katika viwanda vya humu nchini kusafishwa na yale mengine 460,000 huuzwa katika nchi za nje" amenukuliwa Bw. Berouni.
Vuguvugu la kimapinduzi nchini Libya lilisimamisha kabisa biashara ya mafuta nchini humo na shughuli ya uuzaji mafuta katika nchi za nje imerejelewa mwezi September.
Wiki jana, shirika linalodhibiti nishati ambalo makao yake yako Paris Ufaransa lilisema kuwa uzalishaji nchini Libya unarejea kwa kasi zaidi ya iliyotarajiwa baada ya bomba kuu la kusafirisha mafuta kukarabatiwa.
Inakisiwa kuwa zaidi ya asili mia 10 ya miundombinu ya wanachama wa shirika la OPEC iliharibiwa vibaya sana wakati wa mzozo wa miezi minane nchini Libya.
0 Comments