KAMATI Kuu (CC) ya CCM, imemshauri Rais Jakaya Kikwete kukutana na vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni mbali na Chadema aliyokubali kukutana nayo, ili kupanua wigo wa mawazo katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.
Uamuzi huo, kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, umekuja baada ya kutafakari uamuzi wa Chadema kuomba kuzungumza na Rais, kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.
Nape alisema hayo muda mfupi kabla ya mapumziko ya mchana ya wajumbe wa mkutano wa NEC ulioanza jana saa tano asubuhi bila kufafanua nini hasa kilitafakariwa na Kamati hiyo kabla ya kutoa ushauri huo kwa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
"CCM inaamini kuwa majadiliano ndiyo njia bora ya kufikia mwafaka wa mambo mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa ... Chama kinamshauri Rais aangalie uwezekano wa kukutana na vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, ili kupanua wigo wa mawazo katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya," alisema Nape.
Hata hivyo, Chadema kabla ya kuomba wasaa wa kukutana na Rais na kukaribishwa Ikulu, kilipinga kwa nguvu kubwa Muswada huo kwa kuamua kutoshiriki mjadala wake na baadaye kutishia kuitisha maandamano kama kawaida yake nchi nzima.
Tafakuri kwa Chadema Pamoja na Nape kutofafanua kilichotafakariwa ndani ya Kamati hiyo, lakini ilionekana kuwa Kamati hiyo ilitafakari mfululizo wa matukio ya Chadema ya kupinga Muswada huo ndani na nje ya Bunge.
Katika matukio hayo, makada wa Chadema walitoa hoja zilizotafsiriwa na makada wa CCM kuwa ni za upotoshaji wa makusudi, ambazo wakati mwingine walionesha wazi kupinga madaraka halali ya Rais ya kikatiba yanayomruhusu kuunda Tume.
Kudhihirisha kuwa Kamati hiyo ilitafakari matukio hayo ya Chadema, Nape alisema Kamati hiyo pia iliwapongeza wabunge iliowaita wa kutoka vyama vyote vya siasa, kwa kushiriki mjadala na hatimaye kupitisha Muswada wa kuweka utaratibu wa marekebisho ya Katiba wa 2011.
Kauli ya Nape bila shaka, haihusu Chadema na NCCR-Mageuzi, ambavyo havikushiriki mjadala huo wala kupitisha Muswada huo.
CCM yafunga mjadala Katika kile kilichoonekana ni kufunga mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, ambayo Rais anasubiriwa kusaini ili iwe sheria, Kamati hiyo mbali na kupongeza kupitishwa kwa Muswada huo bungeni, iliwaagiza wananchi wahamasishwe kutoa mawazo katika mchakato wa kupata Katiba mpya.
Nape alisema Kamati hiyo iliwaagiza viongozi wote wa CCM, wahamasishe na kuelimisha wananchi kushiriki kipindi chote cha mchakato wa kupata Katiba mpya.
Pia iliwaomba Watanzania washiriki mchakato huo lakini ikasisitiza umuhimu kwao wa kutanguliza uzalendo na upendo wa dhati kwa nchi yao, pamoja na amani na mshikamano ambazo ndizo nguzo na tunu muhimu za Taifa.
Ilimpongeza Rais Kikwete kwa hotuba yake kwa Taifa kupitia wazee wa Dar es Salaam Ijumaa na kuongeza kuwa ilifafanua vya kutosha na kujibu hoja zilizokuwa zinapotosha dhana ya mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.
"Kamati Kuu inaamini hotuba hiyo imewaleta pamoja Watanzania na kuwafanya watambue, kuwa jukumu la kukamilisha uandikaji wa Katiba mpya sasa liko mikononi mwa Watanzania wenyewe," alisema Nape.
Aidha, tofauti na makada wa Chadema wanavyodai, kumtuhumu Spika wa Bunge Anne Makinda, kwa madai ya kuingilia mchakato wa kupata maoni na kuwazuia wasizungumze, Kamati Kuu ilimpongeza Spika na viongozi wenzake wa Bunge kwa jinsi walivyosimamia na kuongoza mijadala ya Bunge na hatimaye kufanikisha kupitishwa kwa Muswada huo.
|
0 Comments