MWANAMKE mwenye umri wa miaka 60, mkazi wa Kibaoni mjini hapa, amewavunja mbavu wasikilizaji wa kesi katika Mahakama ya Mwanzo Ipembe, baada ya kumjibu Hakimu kuwa kijana aliyemfikisha mahakamani hapo si mwanawe bali mumewe.
Katika kesi hiyo, mwanamke huyo Asha Abdallah anamshitaki mumewe, Kiemi Itambu (30), kwa kumwibia Sh 30,000 alizokuwa ameficha chini ya godoro.
Wawili hao wakiwa kizimbani jana, Hakimu Hosea Mkude alimwuliza mke: “Kwa nini wewe bibi unaolewa na kijana ambaye ana umri wa mwanao, huoni aibu?
Asha alijibu: “Mheshimiwa, huyu ni mtoto kwa mama yake aliyemzaa, kwangu ni mume wangu halali ambaye ananitimizia mahitaji yangu yote muhimu.”
Kama vile jibu hilo halikutosha, Asha aliendelea ‘kumpasha’ hakimu: “Kwanza kwa taarifa yako, wako wanawake wengi tu hapa mjini walioolewa na vijana, tena wengine wana vijana wenye umri unaofanana na wa wajukuu zao. Sembuse miye?”
Majibu hayo yalisababisha watu waliojazana kwenye chumba hicho cha Mahakama, washindwe kujizuia na kuangua vicheko.
Ilidaiwa mahakamani hapo, kuwa mshitakiwa Kiemi alitenda kosa hilo Novemba 3, saa mbili asubuhi Kibaoni mjini hapa.
Asha alidai mahakamani hapo kuwa mumewe amekuwa na tabia ya kumwibia Sh 100, 200 na 500, lakini safari hii alivuka mpaka kwa kuiba Sh 30,000 ndiyo maana akaamua kumfikisha mahakamani.
Mshitakiwa alikana mashitaka na yuko nje baada ya kujidhamini mwenyewe kwa ahadi ya kutoa Sh 50,000 hadi Novemba 15 kesi hiyo itakapotajwa
0 Comments