Samuel Eto'o na Eyong Enoh wameitwa na kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot) kutokana na kuchochea mgomo wiki iliyopita.
Mzozo juu ya malipo ulisababisha Cameroon kufuta mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Algeria.
Wachezaji hao wawili wanatazamiwa kufika mbele ya kamati hiyo siku ya Alhamisi, lakini huenda wakaomba shauri lao liahirishwe na kutaka maafisa wa Fecafoot waliohusika nao waitwe mbele ya kamati hiyo ya nidhamu.
Mzozo ulizuka baada ya timu hiyo kucheza mechi mbili dhidi ya Morocco na Sudan, mjini Marrakesh.
Malipo ya marupurupu na fedha wanazolipwa wanapocheza mechi hawakulipwa na wachezaji wakaamua kutokwenda Algeria wakionesha kutoridhika na kunyimwa fedha zao.
Mlinzi wa Tottenham Hotspur Benoit Assou-Ekotto pia ameitwa mbele ya kamati hiyo ya nidhamu kwa kutojiunga na kambi ya timu hiyo kwa ajili ya mchezo dhidi ya Morocco na mechi iliyosusiwa ya Algeria.
Hii si mara ya kwanza kwa Eto'o na Assou-Ekotto kuitwa na kamati ya nidhamu ya Fecafoot mwaka huu.
Mwezi wa Juni Eto'o alionekana hana hatia kwa kutohudhuria mazoezi ya timu ya taifa na kuonesha utovu wa nidhamu kwa kocha wa zamani Javier Clemente.
Wakati huo Assou-Ekotto alionywa kwa kushindwa kujiunga na kikosi cha taifa alipotwa na Clemente kucheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Senegal tarehe 4 mwezi wa Juni.
Waziri wa michezo wa Cameroon Michel Zoah pia ameishutumu Fecafoot kutokana na timu hiyo kushindwa kucheza na Algeria tarehe 15 mwezi wa Novemba.
Zoah ameongeza kusema ujumbe wa watu wanne akiwemo mlinda mlango wa zamani wa timu ya taifa Joseph Antoine Bell, utakwenda Algeria kuomba radhi kwa shirikisho la soka la nchi hiyo pamoja na wizara ya michezo.
0 Comments