MUSWADA wa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Tanzania utakaowasilishwa bungeni hivi karibuni una baraka za pande zote za Muungano, imeelezwa.
Akizungumza jana na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari nchini Ikulu mjini hapa,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein alisema pande hizo zilishirikiana kwa asilimia 100 kuuridhia.
“Katiba mpya ya Tanzania itapatikana mwaka 2014 wakati tukiadhimisha miaka 50 ya
Muungano wetu … tumeshirikiana kwa asilimia 100 kuuandaa muswada wa Katiba hiyo, wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na wa Baraza la Mawaziri la Muungano walikaa pamoja.
“Tulikubaliana pia mimi na Rais Jakaya Kikwete … huu ni muswada wetu sote na utapelekwa
bungeni,” alisema Rais Shein wakati akijibu maswali ya wanahabari hao wakati wa kuadhimisha
mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani.
Dk. Shein alilazimika kutoa majibu hayo kutokana na kuwapo minong’ono, kwamba mchakato
wa Katiba hiyo umekuwa ukipingwa na baadhi ya watu wa upande wa visiwani.
Alisema muswada huo umeandaliwa kwa jitihada za pande zote za Muungano kwa kushirikisha
pia wanasheria wote katika mjadala wa kuangalia ni muswada wa namna gani utakaofikishwa
bungeni ili kutoa fursa kwa wananchi kuchangia mawazo yao.
Alisisitiza kuwa si kweli kuwa Wazanzibari hawautaki na kusema ni jambo jema wakapewa fursa
ya kuujadili waseme wenyewe wanataka Katiba ya aina gani ya kuwaongoza, kuliko masuala
haya kuzungumzwa kiuficho.
Akizungumzia nidhamu kwa baadhi ya watendaji wakuu serikalini, baada ya kulalamikiwa
na wanahabari kuwa wapo wasio na nidhamu wanaokunywa pombe na kudhalilisha nafasi zao
za uongozi, Dk. Shein alisema kama wapo hawastahili kuwa viongozi.
“Mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine serikalini wanaofanya hivyo, hawana sifa za
uongozi … nikiwajua nitachukua hatua dhidi yao.
Alisema viongozi hao walishapewa semina elekezi na hivyo kama wapo wanaofanya vitendo
vya ulevi na kujidhalilisha, wanastahili hatua na kwamba kama ni pombe na kuna ulazima,
basi wanatakiwa kununua na kunywea majumbani mwao na si hadharani.
Pia aliwaonya wanaotumia magari ya Serikali kwa maslahi binafsi, ikiwa ni pamoja na ‘kujirusha’ siku za mwisho wa wiki katika majumba ya starehe, akisema nao walishapewa semina elekezi inayokataza matumizi mabaya ya mali za umma.
Mapema Rais Shein alizungumzia mafanikio na changamoto zilizopatikana katika mwaka
wake mmoja wa urais, akibainisha kupata mafanikio katika sekta za utalii, kilimo, elimu, maji,
afya na ajira kwa vijana na kuwezesha wanawake.
Alisema sekta ya utalii anaipa kipaumbele na kuiita kuwa ni sekta kiongozi, kwa sababu inaingiza asilimia 70 za pato la fedha za kigeni Zanzibar.
Aliahidi katika kipindi kijacho, kuongeza pato la mkulima, kuwezesha vijana kujiajiri kwa
kuwapa zana mbalimbali za kufanyia kazi, ikiwa ni pamoja na kujiunga pamoja na kuanzisha miradi kama ilivyofanyika kwa vijana 600 wanaojiajiri kwa kufanya usafi Unguja.
Kuhusu mazingira, aliahidi kuendelea kupambana na mifuko ya plastiki na kusema haitakiwi kuonekana mitaani, madukani hata majumbani.
Akizungumzia changamoto zilizopo, Rais Shein alizitaja za bei ya mafuta, chakula, kudorora kwa sekta ya benki Ulaya, uharamia katika bahari ya Hindi, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu na kwamba Serikali yake inajitahidi kukabiliana nazo.
Aliahidi kwamba kuanzia sasa atakuwa akizungumza na Taifa kila baada ya miezi mitatu na
kuwataka viongozi wengine kupanga jinsi ya kuzungumza na wananchi kuwaeleza kinachofanywa na Serikali.
0 Comments