Msanii wa Marekani Heavy D, ambaye alikuja kuwa miongoni mwa nyota wa miondoko ya hip-hop katika miaka ya 80, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 44.

Alifariki dunia siku ya Jumanne baada ya kukutwa kapoteza fahamu nyumbani kwake mjini Los Angeles.

Alizaliwa na kupewa jina la Dwight Arrington Myers huko Jamaica mwaka 1967, Heavy D alipata umaarufu mkubwa na bendi yake ya "the Boyz", akitamba na wimbo kama Now That We Found Love.

Alitokea kwenye wimbo wa Jam wa Michael Jackson mwaka 1990 na hivi karibuni aliimba kwenye tamasha la kumkumbuka Jackson huko Cardiff.

Dada yake Jackson La Toya, ambaye aliimba na Heavy D katika tamasha hilo Oktoba 8 alituma rambirambi kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, " Pole zangu ziwaendee familia na wote waliokuwa wakimpenda Heavy D."

Licha ya kujulikana kwa umbile lake kubwa, Heavy D hakukubali mwili wake ndio uwe kielelezo cha sifa yake.


Msanii huyo mwenye haiba mara nyingi alikuwa mchombezaji na mchekeshaji. "Itakuwaje, mimi au TV?" alimkaripia mpenzi wake katika Now That We Found Love, kibao chake kikuu nchini Uingereza.

Aliwa na bendi yake, The Boyz, alianzisha mtindo ulioitwa new Jack Swing- miondoko kadhaa ya R & B- ambayo ilifungua njia kwa wasanii kama Bobby Brown na kundi la Blackstreet.

Albamu zake tatu- Big Tyme (1989), Peaceful Journey (1991) na Nuttin' but Love (1994)- zilifikia kilele cha mauzo yaani platinum nchini Marekani.

Mwanzo wa miaka ya 90, aliimba na wasanii kama vile marehemu Notorious BIG na Janet Jackson.

Muziki wake ulianza kutikisika baada ya kuingia katika fani ya uigizaji, hasa alipoanza kutokea kwenye vipindi kama Law & Order: SVU na Boston Public katika miaka ya karibu ya 2000.

Pia alitokea katika filamu kadhaa, ikiwemo Cider House Rules, na hivi karibuni, akiwa na Ben Stiller na Eddie Murphy kwenye filamu ya kuchekesha ya Tower Heist.

Hata hivyo, aliendelea kuimba na albamu yake ya mwisho, Love Opus, ilionekana kama njia ya kurudi kwenye fani ilipotolewa Septemba mwaka huu.