MCHUNGAJI Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapile ‘Babu Ambi’ (pichani), anaendelea kusakamwa na wagonjwa wanaodai hawakuponyeshwa na dawa yake, wapo walioweka nia ya kumburuza mahakamani lakini mpya ni pendekezo la kumfilisi.
Wanaharakati wameeleza kuwa miongoni mwa mashtaka ambayo wanamfungulia Babu Ambi, mojawapo ni kumfilisi mali zote alizochuma endapo atakutwa na hatia ya ulaghai, wakati wa kutangaza maono aliyopewa na Mungu kuhusu tiba ya kikombe.
Wanadai kuwa Babu Ambi, mkazi wa Kijiji cha Samunge, Loliondo, alitumia matatizo ya Watanzania ya kuugua maradhi sugu ili kujinufaisha, hivyo akatengeneza ulaghai wa tiba ya kikombe kwa maelezo kwamba ni ufunuo aliopewa na Mungu.
Madai hayo yanakuja wakati ambao Babu Ambi ameukata, ameshakamilisha ujenzi wa nyumba yake ya kisasa kijijini Samunge, pia anamiliki magari mawili ya bei mbaya, Toyota Land Cruiser (pick-up) na Isuzu (pick-up).
Babu Ambi, ameshahama nyumba chakavu aliyokuwa anaishi zamani na sasa anaendesha maisha yake kwenye mpya ya kisasa ambayo kwa Samunge, inaonekana ni kama Ikulu kwa jinsi inavyomeremeta.
Wakati Babu alizoea kukanyaga vumbi kwenye nyumba yake ya awali ya udongo, yenye chumba kimoja cha kulala, hivi sasa anatembea juu ya sakafu iliyotandikwa vigae (tiles) kila eneo.
Nyumba ya Babu, pia ina kila kitu ambacho hustahili kuwemo kwenye nyumba ya kisasa yenye hadhi ya mtu mwenye fedha, vile vile ina umeme wa mionzi ya jua na maji ya uhakika.
Mali zote hizo, wanaharakati wanataka zifilisiwe kwa sababu zimepatikana kwa njia ya udanganyifu.
Muungano wa Vyama vya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (Tanopha) ni wanaharakati wa kwanza kutoa tamko la kumburuza mahakamani.
Tanopha wanasema, miongoni mwao, walitumia kikombe cha Babu Ambi lakini hakuna hata mmoja aliyepona.
Wanasema, kila walipokwenda kupima ili waone matokeo ya tiba ya kikombe, majibu yalikuwa ni yaleyale kwamba hakuna mabadiliko.
Wakati Babu alizoea kukanyaga vumbi kwenye nyumba yake ya awali ya udongo, yenye chumba kimoja cha kulala, hivi sasa anatembea juu ya sakafu iliyotandikwa vigae (tiles) kila eneo.
Nyumba ya Babu, pia ina kila kitu ambacho hustahili kuwemo kwenye nyumba ya kisasa yenye hadhi ya mtu mwenye fedha, vile vile ina umeme wa mionzi ya jua na maji ya uhakika.
Mali zote hizo, wanaharakati wanataka zifilisiwe kwa sababu zimepatikana kwa njia ya udanganyifu.
Muungano wa Vyama vya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (Tanopha) ni wanaharakati wa kwanza kutoa tamko la kumburuza mahakamani.
Tanopha wanasema, miongoni mwao, walitumia kikombe cha Babu Ambi lakini hakuna hata mmoja aliyepona.
Wanasema, kila walipokwenda kupima ili waone matokeo ya tiba ya kikombe, majibu yalikuwa ni yaleyale kwamba hakuna mabadiliko.
“Hatuwezi kupoteza muda na fedha zetu kwa kwenda kunywa dawa ambayo haitibu, hii ni kuwarubuni wananchi, wengi wameuza mali zao, wengine kutumia akiba ya fedha walizokuwanazo kwenda Loliondo wakijua wangepona lakini cha kushangaza ni kwamba baadhi yetu wanakufa.
“Wengine wako mahututi baada ya kupewa kikombe, tulikuwa na matumaini ya kupona hadi tuliacha kutumia vidonge vya kurefusha maisha vya ARV, hatuna mengi zaidi ila tunaomba umtafute mwenyekiti wetu akueleza zaidi,” alisema mmoja wa wanachama wa Tanopha.
Mwenyekiti wa Tanopha, Julius Kaaya, aliliambia Uwazi kwa njia ya simu kuwa taasisi yake ilipeleka watu 14 kunywa dawa Loliondo lakini hakuna hata mmoja aliyepona.
“Nakumbuka kwamba kipindi tunaenda huko Loliondo Machi 19, mwaka huu, tulifanya mkutano na waandishi wa habari, tulifika Samunge Machi 22, ambapo Machi 24 walikunywa dawa hiyo kila mmoja akiwa na matumaini ya kupona.
“Baada ya siku 20 tangu wanywe dawa hiyo walienda hospitali kuangalia kama wamepona, daktari aliwaambia hakuna hata mmoja aliyepona, siku 90 baadaye majibu yakawa yaleyale,“ alisema Kaaya.MCHUNGAJI MTIKILA
Naye Mchungaji wa Kanisa la Full Salvation, Christopher Mtikila kwa upande wake amesema kwamba dawa hiyo haitibu na analishughulikia suala hilo ili kumfikisha mahakamani pamoja na mawaziri, wabunge na viongozi wa juu waliokunywa kikombe.
“Mawaziri hao wamewahamasisha wananchi kwenda Loliondo kunywa dawa, lazima tuwashitaki pamoja na viongozi wa dini waliopiga debe,” alisema Mtikila. Viongozi wa dini waliohamasisha ni Askofu Thomas Laizer na Martine Shayo.
Baadhi ya Mawaziri waliopata kikombe ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli. Wengine ni wabunge Augustino Mrema, Edward Lowassa na wakuu wa mikoa Yohana Balele na Abbas Kandoro.
TAMKO LA WIZARA
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Haji Mponda, alisema hivi karibuni kuwa kikombe cha Babu siyo tiba na kwamba wote waliokwenda Loliondo, walipoteza muda.
Kauli ya waziri, ilifuatia ripoti ya uchunguzi wa madaktari bingwa kwamba kikombe cha Babu wa Loliondo, hakitibu.
WABUNGE NAO
Katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 10, baadhi ya wabunge walitaka Babu wa Loliondo achukuliwe hatua kwa sababu dawa yake haitibu.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, alikwenda mbali zaidi kwa kutaka mawaziri waliokwenda Loliondo, wahojiwe na waseme kama wamepona, kwani wao kwa kiwango kikubwa walihusika kupotosha umma.
UTETEZI WA BABU
Kwa upande wa Babu Ambi, ameendelea kushikilia msimamo wake kuwa dawa yake imeponyesha wengi.
“Kama hawajapona siyo makosa yetu. Tuliwaambia kabla kuwa katika tiba hii kigezo cha kwanza ni kuwa na imani na hapa tuna uthibitisho wa kutosha wa watu walioponywa na maajabu ya dawa hii wakiwemo wagonjwa wenye Ukimwi,” alisema Babu Ambi na kuongeza kuwa anapigwa vita na wengi kwa sababu ya wivu.
Kuhusu utajiri wake, alisema kuwa yeye hana mamilioni ya fedha kama inavyodaiwa ila akakiri kumiliki nyumba ya kisasa pamoja na magari mawili ambayo amesema yanamsaidia kubeba dawa pamoja na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Loliondo.
KUHUSU KIKOMBE
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu wa KKKT Arusha, Thomas Laizer, zaidi ya watu milioni tatu wameshatibiwa Loliondo.
Kila mgonjwa alikuwa analipa shilingi 500, hivyo kwa hesabu ya watu milioni tatu, maana yake kikombe kimeshaingiza zaidi ya shilingi bilioni 1.5.
0 Comments